January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kiwanda cha kukoboa kahawa chateketea Karagwe. Picha na Ashura Jumapili, Timesmajira

Kiwanda cha Kahawa chawaka moto

Na Ashura Jumapili, Karagwe

KIWANDA cha kukoboa kahawa kilichopo Wilayani Karagwe mkoani Kagera kinachomilikiwa na mfanyabiashara, Karim Amri, kimeteketea kwa moto na kusababisha hasara ya zaidi ya sh. bilioni 2, huku chanzo cha moto huo kikiwa hakijafahamika na  uchunguzi unaendelea.

Moto huo ulianza kuteketeza kiwanda hicho kuanzia alfajiri saa 11 alfajiri jana kabla ya Zima Moto kufika eneo la tukio na kuanza kukabiliana nao.

Baadhi ya wananchi walioko karibu na kiwanda hicho walifanya jitihada za kuuzima moto huo ili usiendelee kuleta madhara zaidi kwa kutumia maji na mchanga, lakini walizidiwa nguvu na moto huo.

Sehemu ya kiwanda ilivyoteketezwa na moto. Picha na Ashura Jumapili, Timesmajira

Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Godfrey Mheruka akizungumza na Majira alisema mitambo 21 ya  kiwanda hicho imeteketea kwa moto.

Mheruka alisema kuteketea kwa mitambo hiyo kumeisababishia kiwanda kupata hasara ya zaidi ya sh. bilioni 2 kwa mmiliki wa kiwanda hicho.

“Kutokana na ajali za moto kutokea mara kwa mara wilayani hapa, kama wilaya tumeishaanza kuweka tahadhari kwa kuanza ujenzi mkubwa wa kituo cha Zima Moto na wananchi wameweka nguvu zao tuko katika hatua ya kupaua na jengo litagharimu sh. milioni 30 tumeishapata mashine na tunajiandaa kununua gari la zima moto,”alisema Mheruka

Alisema viwanda vyote vinatakiwa kuwa na bima ili vinapopata ajali viweze kulipwa fidia kutokana na bima walizonazo.

Kamanda wa Jeshi la Zima Moto na Uokoaji mkoani Kagera, Hamis Dawa, alisema kiwanda hicho kimeteketea kwa moto ambao unadhaniwa kusababishwa na shoti ya umeme au radi kutokana na mvua iliyokuwa inanyesha usiku wa kuamkia jana.

Dawa aliongeza kwamba Majira ya saa 12 :23 asubuhi alipata taarifa kuwa kiwanda cha kahawa cha Karimu Amri Amir kinawaka moto na kutuma gari la zimamoto kutoka Bukoba kwenda Karagwe, hivyo majira ya mchana walifanikiwa kuzima kabisa moto huo.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Eliabu Josephat alisema yeye alikuwa anapita eneo la kiwanda na ndipo alisikia kelele za watu kuomba msaada wa kuzima moto na muda huo waliwasiliana na zimamoto wilaya ya Karagwe ambaye aliwataarifu upande wa mkoa.