Na Bakari Lulela,Timesmajira, Oline
KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu, kimelaani mauaji ya kikatili ya mtoto, Nyanzobhe Mwandu (4) yaliyotokea Juni 16 mwaka huu mkoani Tabora baada ya nyumba aliyokuwa akiishi kuchomwa moto.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na kituo hicho, mauaji hayo yametelezwa baada ya maagizo ya kuchoma nyumba za wanakijiji, ambao wanazunguka Hifadhi ya Kijiji ya Ngitiri.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga amesema mauaji hayo ni kinyama yanafaa kulaaniwa kwa nguvu zote.
“Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, kinalaani kitendo hicho na kutaka wahusika wa mauaji hayo kuchukuliwa hatua za kisheria, kutokana na ukiukwaji wa katiba ya nchi na pia haki za binadamu ambapo ndugu wahabari ibara ya 24 (1) ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 kama ilivyofanyiwa marekebisho ,inasema kila mtu anayo haki ya kumiliki mali na haki ya hifadhi ya mali yake aliyonayo kwa mujibu wa sheria,” amesema.
Ameongeza kuwa ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, pamoja na marekebisho yake inatamka wazi kwamba kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kwa jamii hifadhi ya maisha yake kwa mujibu wa sheria.
Ameiomba Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), ihakikishe mipaka yote ya vijiji vinavyopakana na ardhi ya hifadhi, inawekwa bayana ili wananchi wafahamu mipaka ya vijiji vyao ilipoishia pamoja na kuhakikisha vijiji visivyoathirika na amri vinabaki salama na wananchi waruhusiwe kuanza kuvuna mazao yao.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Uchechemuzi wa Maboresho LHRC, Joseph Oleshangay amesema kumekuwa na matukio mengi ya kikatili na kuitaka serikali iendelee kuchukua hatua ili kukomesha vitendo hivyo vya kikatili vinavyofanwa na baadhi ya watu.
“Kuna matukio mengi ya kikatili yanayofanywa na baadhi ya watu, hivyo tunaitaka serikali na mamlaka zingine ziendelee kuchukua hatua ili kukomesha matukio hayo,” amesema Oleshangay.
More Stories
Prof.Mwakalila awafunda wanafunzi wapya MNMA juu ya uadilifu,uzalendo
Kapinga asema mafanikio katika sekta ya nishati yanatokana na jitihada za Rais Samia
Bumbuli kutekeleza miradi kwa kuangalia vipaumbele