Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Njombe
MBIO za Kitulo Garden(Kitulo Garden Marathon), zimezinduliwa rasmi mkoani Njombe na zinatarajia kufanyika Mei 2,2026 katika Hifadhi ya Taifa ya Kitulo,
Mbio hizo zimezinduliwa Januari 8,2026 na Ofisa Michezo wa Mkoa wa Njombe, Flavian Kitago kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Anthony Mtaka ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo.

Amesema mbio hizo ni za kipekee nchini, zikielezwa kufanyika katika uwanda wa juu kuliko mbio zote nchini, hali ambayo itawapa washiriki utofauti wa kimazingira na hali ya hewa ya kitofauti.
Kitago amesema,uongozi wa Mkoa wa Njombe umefurahishwa kuanzishwa kwa mbio hizo ambazo zitakuwa chachu ya maendeleo mkoani humo na hamasa ya utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Kitulo.
Pia amesema mbio hizo ni za kwanza kufanyika katika Mkoa wa Njombe,hivyo ametumia nafasi hiyo kuwahimiza wadau wote wa maendeleo mkoani humo na nchini kutumia fursa hiyo kujitangaza.
Hivyo Mkoa utashirikiana na kamati ya mandalizi ya Kitulo Garden Marathon huku akiwakaribisha wageni kutoka pande zote za nchi na nje ya nchi kushiriki kwa wingi kwa kuhakikisha usalama wao wakati wa mbio hizo.
Kwa upande wake Msimamizi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Kitulo, Harry Gazi,amesema hifadhi hiyo hutambulika kimataifa kama hifadhi ya upendo, ambapo mwaka 2025 imeshinda tuzo ya Afrika kama kituo bora cha fungate (Africa’s Best Honeymoon Destination), huku ikiingizwa katika kinyang’anyiro hicho hicho katika mashindano ya kidunia.
“Napenda kutumia fursa hii kuwakaribisha wageni kutoka pande zote za nchi kuja kutembelea hifadhi ya kitulo, na pia kuitumia Marathon hii kama njia yao ya kufika na kufurahia urithi huu wa dunia wa kipekee wa hifadhi hii,”amesema Gazi.
Akizunguza kwa niaba ya kamati ya maandalizi ya Kitulo Garden Marathon, Monny Luvanda,amesema mbio hizo zinalenga kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhamasisha na kukuza utalii nchini ambazo alizianzisha kupitia program ya Royal Tour.
Pia amesema mbio hizo zinaelenga kuigusa jamii ambapo sehemu ya mapato yake yameelezwa kuchagia huduma za elimu na afya.
Hata hivyo amesema mbio hizo ni “Full Marathon” ambazo zitajumuisha kilomita 42, kilomita 21.5, kilomita 10 na kilomita 5 huku zikitanguliwa na mbio za hiari za baiskeli (Cycling Fun Race) itayofanyika siku moja kabla Mei Mosi 2026 huku waendesha baiskeli kujumuika na washiriki wa Marathon eneo la Kitulo Campsite Mei 2,2026.

Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Riadha Mkoa wa Njombe, Tegemea Mbogela,amewasihi wanariadha na wapenda michezo nchini kote kushiriki kikamilifu katika mbio hizo ambayo itaweka historia ya kipekee kwao.
Meneja wa Huduma kwa Wateja wa NMB Makete, Elinkaila Nashokigwa, ameeleza kuwa benki hiyo inaona fahari kuwa mdhamini mkuu wa mbio hizo ambazo zinaenda kufungua fursa na kuwezesha huduma za jamii kitu ambacho kinaenda sambamba na sera za benki yao.
Naye Adam Akaro ambaye alimuwakilisha Meneja wa CRDB Bank Tawi la Ikonda, Makete alieza kuwa CRDB Bank imefurahi kuwa miongoni mwa wadhamini wakuu wa mbio hizo ambao utamuwezesha kufikisha huduma zake kwa jamii na kugusa maisha ya wengi wilayani Makete.

Ada ya ushiriki imeelekezwa kuwa shilingi 40,000 ambayo utaweza kujisajili huku wageni kutoka nchi za nje wakilipa ada ya dola za kimarekani 40, kiwango ambacho kitamwezesha mshiriki kujipatia Marathon Kit, Medali, namba ya BIB pamoja kugharamia gharama za kuingia hifadhini.
Sambamba na hayo, uzinduzi huo ulibarikiwa kwa maombi yaliyoongozwa na Askofu Stephen Nguvila wa Kanisa la Kiinjili la Kiluther Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kusini Magharibi, ambaye aliambatana na Msadizi wa Askofu Mch. Christon Ngogo.

More Stories
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi
Waziri Mkuu kuanza ziara mkoani Rukwa Marchi 8 Hadi 10
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani