Na Joyce Kasiki,Timesmajira online Dodoma
NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula na Naibu Waziri Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Deus Sangu , wamepongeza juhudi za Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Wakizungumza na waandishi wa habari Juni 20,2025 katika maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma katika banda la REA ,Manaibu Waziri hao wamesema, hatua hiyo ni muhimu si tu kwa kulinda afya za wananchi bali pia kwa kuhifadhi mazingira ya Taifa.
Kwa upande wake Naibu Waziri Kitandula amesema kuwa matumizi ya nishati safi ni hatua madhubuti katika kukabiliana na changamoto ya ukataji miti usio endelevu ambao unasababisha athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Wizara ya Maliasili na Utalii imepewa jukumu la kulinda rasilimali za misitu. Kumekuwa na changamoto kubwa ya ukataji miti ovyo kwa ajili ya kuni na mkaa. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuliona hili na kuanzisha Mkakati wa Kitaifa wa matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia,” amesema Kitandula na kuongeza kuwa
“Mbali na kuokoa maisha ya kina mama wanaotumia nishati chafu, mkakati huu utasaidia kulinda mazingira yetu. Ni wajibu wetu kama viongozi kuhamasisha Watanzania kuitikia kampeni hii ili Taifa letu libaki salama kwa vizazi vya sasa na vijavyo,”
Naye Naibu Waziri Sangu, ameeleza kuridhishwa kwake na ushiriki wa REA katika maadhimisho hayo, akisema kuwa taasisi hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kuboresha maisha ya wananchi kwa kuwapelekea huduma ya umeme vijijini pamoja na kuendeleza kampeni ya nishati safi ya kupikia.
“Kwanza niwapongeze REA kwa kushiriki katika maadhimisho haya ambapo wananchi wanapata fursa ya kufahamu miradi mnayoitekeleza,
“Juhudi zenu katika kutekeleza ajenda ya nishati safi ya kupikia, ambayo ni kipaumbele cha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, zinastahili pongezi.
“Endeleeni kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kutumia nishati safi kwa ajili ya afya na mazingira bora,” aliongeza.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi