February 21, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kitabu cha maadili ya Kitanzania kwa watoto chazinduliwa

Na Imma Mbuguni, TimesMajira Online, Dar es Salaam

KATIKA jitihada za kuhifadhi na kuthamini kizazi chenye maadili na makuzi bora,mwandishi Mtanzania amezindua kitabu cha kwanza katika mfululizo wa vitabu vya watoto, vyenye maudhui na falsafa ya utamaduni wa Kitanzania na Afrika, kikiwa na lengo la kupanua mawazo ya mtoto wa kitanzania.

Akibainisha malengo hayo katika hafla ya uzinduzi wa kitabu cha Jua na Ua iliyofanyika jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa wiki na kuhudhuriwa na wadau pamoja na wapenzi wa vitabu kutaka maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, mwandishi wa kitabu hicho, Prudence Zoe Glorious, alisema kuwa lengo ni kuwawezesha watoto wetu kurithi tamaduni zetu za kitanzania.

“‘Jua Na Ua’ ni kitabu kinachochanganya falsafa ya Kitanzania na utamaduni wa Kiafrika, zenye lengo la kukuza mawazo ya watoto, kuamsha picha za kimwili na kiakili, na kuwaelekeza watoto katika hadithi zinazobeba hekima na urithi wa tamaduni za Kitanzania” alisema Zoe.

Akieleza ‘Jua Na Ua’, Zoe alisema kuwa ni kulenga mkusanyiko wa hadithi za kuvutia ambazo zitakazowafundisha watoto mambo muhimu ya maisha huku wakijivunia mizizi yao ya kitanzania na Kiafrika pamoja na maadili ya jamii zao.

Wahusika wakuu katika kitabu hiki ni wawili: wa kwanza ni Jua, anaye mwakilisha mtoto wa kiume wa Kiafrika, na Ua, anayemwakilisha mtoto wa kike wa Kiafrika. Watoto hawa wawili wanalelewa katika familia ya Kitanzania inayoshikilia maadili na desturi za Kiafrika.

Kitabu cha ‘Jua Na Ua’ kinajumuisha kurasa 24, kila moja ikiwa na simulizi inayotoa mafunzo ya kimaadili kwa watoto ambapo miongoni mwa maudhui hayo ni pamoja na fikiri mawazo mazuri kwa ajili yake na wengine, kwenda pamoja na wengine, kuzungumzia zaidi unachojali pamoja na marafiki wanavyokuzunguzia kutokana na wanavyokutazama.

Mambo mengine ni kuhusu kuwa na hamu ya kuendelea kujifunza zaidi, kuunganisha mambo mbalimbali, huruma na kupata uwanda mpana zaidi wa michezo. Mwisho kitabu hicho kinalenga kumsaidia mtoto kuwa na uwezo wa kupaza sauti na kufikisha ujumbe kwa watu wote.

Aidha kitabu hicho kinatoa picha ya jinsi watoto wa Kitanzania na wanavyoshiriki katika mambo mbalimbali katika familia zao na namna wanavyotumia muda wao wanapokuwa nyumbani au wakati wa likizoni, mbali na masomo na kazi za shule.

‘Jua Na Ua’ inasisitiza umuhimu wa wazazi kutumia muda pamoja na watoto wao, kutembelea mbuga za wanyama ili kuona wanyama kama vile nyani wanaoshuka kutoka mti hadi mti, simba wakilamba na kutembea kwenye majani ya rangi ya kahawia, zebra zenye mistari ya kipekee, lakini zaidi, twiga – anayekua kwa urembo na kutembea kwa heshima.

Sherehe ya uzinduzi ilifanyika katika ofisi ya PZG-PR, ambapo wageni walipata fursa ya kuzungumza na mwandishi wa kitabu hicho, ambaye pamoja na mambo mengi alieleza kuhusu mchakato wa uandishi wake na umuhimu wa kuandika kwa ajili ya kizazi kijacho.

Prudence Zoe Glorious, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa PZG-PR, alisisitiza dhamira yake ya kukuza mawazo na picha za watoto wa Kitanzania kupitia fasihi na usomaji wa vitabu, shauku ambayo imemuweka kuwa kiongozi maarufu katika nyanja za fasihi na uhusiano wa umma.

“Uwaki wa uwakilishi katika vyombo vya habari mbalimbali ni muhimu. Nilikuwa na hamu ya kuunda kazi ya fasihi ambapo wahusika wakuu ni watoto wa Kiafrika ili kuonyesha picha nzuri ya Uafrika kwa kuingiza falsafa zetu na urithi wetu katika hadithi tunazozisimulia kwa watoto wetu.

‘Jua Na Ua’ inaheshimu hekima ya Tanzania, ikiwahamasisha watoto kufikiria kwa kina, kukumbatia urithi wao, na kuchunguza uwezo wao. Inachochea pia imaginaisho, na kama tunavyofahamu, imaginaisho ni aina ya juu ya akili,” alisema.