November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kiswaga: Serikali inajitahidi kutatua changamoto ya maji,umeme

Na Daud Magesa, Timesmajira Online,Magu

Mbunge wa Jimbo la Magu mkoani Mwanza Boniventure Kiswaga amesema changamoto za maji na umeme zimesababishwa na ongezeko la watu hivyo serikali inajitahidi kuzitatua kwa kuwafikishia wananchi huduma hizo ingawa haiwezi kuzitatua zote kwa wakati mmoja.

Kiswaga ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi katika mikutano ya hadhara vijiji vya Kitumba, Igekemaja, Buseka na Kanyama wilayani humo, amesema yeye, Madiwani na Wenyeviti wa serikali za mitaa ni chombo cha kubeba kero na changamoto za wananchi na kuzifikisha panapo husika kwa utatuzi hatimaye wapate maendeleo.

“Hakuna jambo gumu kama elimu naomba mtuamini,serikali inafanya kazi kuhakikisha changamoto zote zinatatuliwa na maendeleo yanapatikana,suala la uhaba wa madawati wananchi changieni,tuwanusuru watoto na adha ya kukaa chini,”Kiswaga.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Magu,Enos Kalambo amesema uchaguzi wa serikali za mitaa ni maandalizi ya uchaguzi mkuu 2025, hivyo wananchi wasisahau kukichagua Chama Cha Mapinduzi ili waendelee kula matunda ya maendeleo yanayoletwa na serikali.

Amesema miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa weledi na viwango ni kwa sababu ya umahiri na usimamiza wa fedha wa viongozi waliopo madarakani.

Naye Katibu wa CCM Wilaya ya Magu Fratha Katumwa amesema kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa,wananchi wajitokeze kuboresha taarifa zao katika daftari la wapiga kura ifikapo Agosti 21 hadi 27,mwaka huu na ambao hawajajiandikisha hasa vijana wafanye hivyo ili wapate sifa ya kuchagua viongozi wao.

Awali Diwani wa Kata ya Kisesa Joseph Kabadi amesema serikali imeleta fedha sekta ya elimu milioni 168 za ujenzi wa madarasa na matundu ya vyoo vya shule Msingi Kitumba,Mondo milioni 50 za ujenzi wa madarasa mawili mapya huku saruji mifuko 200 ikitolewa na Chuo Cha Mipango.