January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

KIST, Chuo cha AP Hogeschool Antwerpen watiliana saini kukuza ushirikiano Sekta ya Elimu


Na Haji Mtumwa, Zanzibar

Taasisi ya Karume Sayansi na Teknolojia Zanzibar (KIST)  imesaini Hati ya makubaliano ya pamoja  na Chuo Cha AP  Hogeschool Antwerpen kutoka Belgium kwa lengo la kukuza ushirikiano baina ya Taasisi hizo katika Sekta ya Elimu.

Hafla hiyo ya Utiaji Saini ilifanyika Chuoni hapo Mbweni Mjini Zanzibar baina ya Mkurugenzi wa Taasisi ya Karume Sayansi na Teknolojia , Dkt Mahmoud Abdulwahab na Bwana Tom Peeters ambae ni Mwakilishi wa Chuo Cha AP Hogeschool Antwerpen kutoka Belgium.

Akizungumza katika hafla hiyo Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Dkt Mahmoud Abdulwahab alisema, makubaliano hayo yaliyofanyika yamezingatia katika mambo matatu ikiwemo mabadilishano ya Wanafunzi na wataalamu, mabadilishano ya Wakufunzi kwa lengo la kujifunza, pamoja na kupata maandiko yatakayowezesha kukipa hadhi chuo hicho.

Alieleza kuwa makubaliano hayo yatasaidia kwa kiasi kikubwa katika kukuza ubora wa Chuo kupitia maandiko yatakayofanyika na kupatikana kupitia makubaliano hayo.

Aidha Dkt Mahmoud alisema atahakikisha kuwa makubaliano hayo yanafanyiwa kazi na kuzaa matunda yanayotarajiwa na kuwawezesha katika kuanzisha miradi ya pamoja baina ya Taasisi hizo.

Katika hatua nyengine Dkt Mahmoud aliueleza Ujumbe huo kuwa Zanzibar hivi sasa inaendelea na utekelezaji wa sera ya Uchumi wa buluu hivyo umefika wakati wa kuitumia Sayansi na Teknolojia katika kufanikisha Uchumi wa buluu.

“Tutahakikisha tunamsaidia Rais kupitia Tekonolojia katika kufanikisha na kukuza Uchumi wa Buluu kwani Sayansi inamchango mkubwa katika kufanikisha Uchumi huo”, alisema Dkt Mahmoud.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Chuo cha AP Hogeschool, Tom Peeters alisema makubaliano hayo yatakuza uhusiano baina ya Belgium na Zanzibar katika Teknolojia, pamoja na kusaidia katika kuwaandaa Wanafunzi wa Taasisi mbili hizo  katika mazingira ya kazi.

Aidha alisema wameweza kutizama mazingira ya Zanzibar kwa kiasi kikubwa na kuona ipo haja ya kukuza ushirikiano baina ya Taasisi hizo ili kukuza Teknolojia kwani nchi ya Belgium imepiga hatua kubwa katika Teknolojia hivyo ipo haja ya kukuza na kuendeleza ushirikiano.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia Zanzibar (KIST) Dkt. Mahmoud Abdulwahab Alawi akizungumza katika hafla ya utiaji saini Hati ya makubaliyano ya pamoja baina ya Taasisi yake na Chuo cha AP  Hogeschool Antwerpen kutoka Belgium, kwa lengo la kukuza na kubadilishana uzoefu baina ya Taasisi hizo, hafla iliyo fanyika Ukumbi wa Dkt. Idrissa Muslim Hija, Mbweni Mjini Zanzibar.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia Zanzibar (KIST) Dkt. Mahmoud Abdulwahab Alawi akizungumza katika hafla ya utiaji saini Hati ya makubaliyano ya pamoja baina ya Taasisi yake na Chuo cha AP  Hogeschool Antwerpen kutoka Belgium, kwa lengo la kukuza na kubadilishana uzoefu baina ya Taasisi hizo, hafla iliyo fanyika Ukumbi wa Dkt. Idrissa Muslim Hija, Mbweni Mjini Zanzibar.
Baadhi ya Wakufunzi wa Taasisi ya Karume Sayansi na Teknolojia Zanzibar (KIST),wakiwa katika picha ya pamoja  na Ujumbe kutoka Chuo cha AP  Hogeschool Antwerpen kilichoko Belgium, mara baada ya hafla ya utiaji saini  hati ya makubaliano ,(katikati) ni Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Dkt. Mahmoud Abdulwahab Alawi hafla iliyo fanyika Ukumbi wa Dkt. Idrissa Muslim Hija, Mbweni Mjini Zanzibar