January 29, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kishindo Mkutano wa Nishati leo, kesho Dar

*Kuhudhuriwa na marais 24 wa nchi za Afrika, wafanyakazi wa umma Dar kufanyia kazi nyumbani, watakaohitajika kazini wawekwa hadharani

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline

MKUTANO wa Wakuu wa Nchi za Afrika Kuhusu Nishati (Africa Energy Summit) unaaza leo ukitarajiwa kumalizika kesho, ambapo kwa siku hizo mbili watumishi wa umma wametakiwa kufanyia kazi zao nyumbani isipokuwa wale ambao mazingira ya kazi yao yanawahitaji.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi, imeeleza kuwa wafanyakazi watakaotakiwa kufika maeneo yao ya kazi ni wale ambao mazingira ya kazi zao yanawahitaji kuwa katika vituo vya kazi kama vile watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama, sekta ya afya, na sekta ya usafiri na usafirishaji.

Taarfia hiyo imewasahauri waajiri katika sekta binafsi kuwaruhusu watumishi wao kufanya kazi nyumbani au kuweka mipango ya kuepuka changamoto za usafiri zinazoweza kutokea kutokana na kufungwa kwa barabara.

Hatua hiyo inakuja kutokana na mkutano huu kutarajiwa kuwa na ugeni mkubwa, ambapo baadhi ya barabara muhimu za Jiji la Dar es Salaam zitafungwa kama ilivyotangazwa na Jeshi la Polisi.

Ili kuepuka usumbufu, Serikali imetoa mwongozo kwa watumishi wa umma katika Mkoa wa Dar es Salaam kufanya kazi nyumbani tarehe 27 na 28 Januari, 2025.

Tanzania imepata heshima kubwa ya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika Kuhusu Nishati (Africa Energy Summit) utakaofanyika jijini Dar es Salaam leo na kesho.

Mkutano huu unaandaliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania, Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika.

Katika mkutano huu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, atakuwa mwenyeji wa Marais 24 kutoka nchi za Afrika, wawakilishi wa Wakuu wa Nchi na Serikali 21, na Wakuu wa Taasisi za Kimataifa sita, wakiwemo Rais wa Benki ya Dunia, Rais wa Benki ya Afrika, na Rais wa Taasisi ya Rockefeller.

Aidha, washiriki 2,600 kutoka ndani na nje ya Tanzania wamejisajili kushiriki katika tukio hili kubwa.

Aidha taarifa hiyo imeeleza kuwa, kuwa benki hazitafungwa, na biashara katika Soko la Kariakoo zitaendelea kama kawaida. Hoteli na migahawa pia haitafungwa, na shughuli za kibiashara katika maeneo hayo zitakamilika kama ilivyopangwa.

Mkutano huu wa Afrika kuhusu Nishati unalenga kukuza ushirikiano kati ya nchi za Afrika na taasisi za kimataifa katika sekta ya nishati, na unatarajiwa kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya nishati barani Afrika.