November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kishindo cha Membe kurejea CCM, Shaka aongoza mapokezi

Na Mwandishi wetu, TimesMajira, Online

ALIYEKUWA mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Bernard Membe ameeleza sababu zilizomfanya arejee CCM ikiwemo kuondoka kwa sababu ambayo ilimfanya atimkie upinzani.

Aidha, amefungunguka jinsi alivyoumia kutokana na uamuzi wa kumwondolea uanachama wa CCM, Chama alichokulia huku akiahidi sasa atafia ndani ya CCM.

Akizungumza katika mkutano huo, katika Kijiji cha Rondo, alisema Machi 30 hadi Aprili 1, mwaka huu aliitwa Dodoma, kwenye Mkutano wa Kamati Kuu ya Maadili na Mkutano Mkuu wa Halmashauri Kuu, alipewa nafasi na Mwenyekiti wa CCM Taifa kuzungumza na wana CCM.

“Mama yetu, Rais wetu na Mwenyekiti wetu wa CCM Taifa alinipa nafasi ya kuzungumza na wajumbe wa kamati kuu ya Chama Taifa. Nashukuru kwa kupewa nafasi ile na wajumbe waliliridhia kwa kauli moja nirejee CCM.

“Nimerejea CCM kwa sababu kuu mbili, sababu ya kwanza nilishauriwa na viongozi wa dini zote, nilishauriwa na viongozi wa CCM ngazi ya Wilaya na Mkoa, nilishauriwa na marafiki zangu wote nirejee CCM, nilishauriwa na wana CCM.

“Kutokana na ushauri wote huo sikuwa na namna nyingine zaidi ya kutii, nimekubaliana na ushauri wa wote waliosema nirudi CCM na sasa nimerudi CCM,” amesema Membe.

Amesema sababu ya pili ya kurudi kwenye Chama hicho inatokana na dhamira yake ya kukitumikia Chama Cha Mapinduzi hadi atakapokwenda kaburini. “Nilipoondolewa CCM nilisikitika sana, nilisonekana sana, na ninyi wananchi mlisikitika, mlisononekana.

“Sababu ambazo zilinifanya niondoke CCM haziko tena, narudi sababu zilizoniondoa CCM haziko tena. Nimerudi, namshukuru Mwenyekiti wa CCM na wajumbe wa Kamati Kuu kunirudisha. Nimerudi kwenye Chama ambacho nimezaliwa na kukulia, chama ambacho kimenisomesha.

“Hivyo niahidi sitaondoka tena, nitabakia CCM hadi mwisho wa uhai wangu. Kurudi kwangu CCM nitaendelea kukitumikia Chama changu na sasa nitaendelea kushirikiana na Mbunge wangu Nape Nnauye. Mwaka 2015 nilisema nitawaletea Nape na kweli nilimleta, hivyo sasa Mtama mtakuwa na wabunge wawili, Mbunge wetu Nape na mimi mbunge wa chini chini.”

Akizungumza katika mkutano huo, Shaka amesema Memembe amerejeshwa katika Chama baada ya kufuatwa kwa utaratibu ikiwemo kujadiliwa na tawi lake na vikao vya juu.

Shaka amesema Membe na wanachama wengine zaidi ya 1,670 waliovuliwa uanachama ambao wamejadiliwa katika vikao na kurejeshewa uanachama, sasa wanaweza kukabidhiwa kadi zao katika matawi yao.

Shaka amesema kurejea kwa Membe ndani ya CCM kuendelee kuwa chachu ya kudumisha umoja na mshikamano hususan kwa wanaccm wa Jimbo la Mtama.