Na Penina Malundo,Timesmajiraonline, Pwani
MKUU wa Wilaya ya Kisarawe, Petro Magoti, amesema maandalizi yamekamilika ya kusherehekea siku ya mfanano wa tarehe ya kuzaliwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, ifikapo Januari 27, 2025 katika wilaya yake.
DC Magoti aliyasema hayo jana Mkoani Pwani wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika ofisini kwake .
Alisema watu wa Kisarawe wamejipanga kusherehekea ‘Birthday” ya Rais Samia ambaye ni hodari na mchapakazi.
“Katika sherehe hii tutakata keki na kusherehekea pamoja na wananchi wa Kisarawe huku tukimuombea dua njema kwa Mwenyeezi Mungu azidi kumpa afya na umri ili aweze kulitumikia taifa lake “alisema DC Magoti.
Wakati huo huo alisema Januari 25 asubuhi kutafanyika uzinduzi wa wiki ya sheria utakaofanyika kwenye Uwanja wa Chanzige Wilayani Kisarawe Mkoa wa Pwani ambapo huduma ya kisheria itaendeshwa kwa wiki moja huku kilele chake kikifanyika Februari mosi .
Alisema huduma za Kimahakama zitafanyika kwenye Kata zote za Kisarawe huku wananchi ambao wanakabiliana na migogoro ya ardhi, mirathi, ndoa na mengineyo wamepewa wito wa kujitokeza kupata huduma hiyo adhimu.
“Huduma hii ya kisheria itatolewa kuanzi saa moja asubuhi hadi jioni,” alisema DC Magoti.
Wakati huo huo, DC Magoti alitoa onyo kali kwa wazazi ambao hawawapeleki watoto shule bila ya kuwa na sababu maalumu kwamba watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
Naye Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi wa Mahakama ya Kisarawe, Emmy Nsangalufu alisema kuwa wiki ya sheria itaanza Januari 25 hadi 31, mwaka huu pia kutakuwa na gari ambalo litakuwa mfano wa Mahakama inayotembea huku lengo likiwa kuwafikia wananchi na kuwapa huduma wanayostahili.
Nsangalufu alitoa wito kwa wananchi kuwa Mahakama ni mali ya wananchi, hivyo waitumie kwa manufaa yao na siku ya uzinduzi wataanza na maandamano asubuhi kwenda kukutana Uwanja wa Chanzige.
” Tumejipanga kuwafikia wazee na watu wote wasiojiweza ndani ya kata zote 17 tutakuwa na gari pamoja na Mawakili wabobevu katika kutatua shida zao,” alisema Nsangalufu.
More Stories
Waislamu Mwanza wapokea Ramadhani kwa maandamano ya kidini
Kamati ya kudumu ya Bunge ya utawala,katiba na sheria yaridhishwa ujenzi soko Kariakoo
TRA Tanga yakusanya bil.178.3 kwa miezi sita