December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

‘Kipyenga’ chapulizwa uchaguzi mashirika yasiyo ya kiserikali

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Kamati ya Mpito ya Kuratibu Uchaguzi wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali imetoa wito kwa viongozi na wanachama wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi wa Baraza kuanzia katika ngazi ya Wilaya, Makundi Maalum, Mkoa hadi Taifa.

Wito huo ulitolewa na Mwenyekiti Kamati ya Mpito ya kuratibu uchaguzi wa Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya kiserikali, Christina Ruhinda wakati akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu mchakato wa uchaguzi wa wajumbe wa Baraza la mashirika yasiyo ya kiserikali (NACONGO) Jana Jijini Dar es Salaam ambapo alisema kwa mujibu wa kanuni ya 5(a), 5 (b) (ii) na 5(c)(v) ya kanuni za uchaguzi za Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya kiserikali za mwaka 2016, Baraza linawataka kufanya uchaguzi Kila baada ya miaka mitatu.

Ruhinda alisema sifa za mgombea wa nafasi za uongozi ni pamoja na kuwa kiongozi au mwanachama katika shirika lisilo la kiserikali lililosajiliwa chini ya sheria ya mashirika yasiyo ya kiserikali na mwenye uzoefu na uelewa mpana wa sera, sheria, kanuni na miongozo ya mashirika yasiyo ya kiserikali

Pia alisema “Mgombea awe Mtanzania isipokuwa kwa mwakilishi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya Kimataifa lakini mwenye kibali cha kufanya kazi Tanzania, awe na umri usiopungua miaka 18 na usiozidi miaka 70, asiwe alishawahi kupatikana na makosa ya jinai awe na elimu ya kidato cha nne au zaidi, awe na uwezo mzuri wa kuzungumza lugha ya Kiswahili na Kiingereza pia awe na akili timamu.”

Kuhusu vigezo vya Shirika Kushiriki katika Uchaguzi Ruhinda alisema Shirika linatakiwa liwe limesajiliwa kwa mujibu wa Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Sura ya 56 ya Sheria za Tanzania lakini pia liwe linatekeleza shughuli zake katika eneo au afua husika.

Pia alisema “Shirika liwe katika orodha ya Msajili Msaidizi wa Halmashauri/Wilaya au Mkoa husika, liwe linatekeleza shughuli zake kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo inayosimamia Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, ikiwemo ulipaji wa ada na uwasilishaji wa taarifa, kila Shirika Lisilo la Kiserikali lililokidhi vigezo tajwa hapo juu litakuwa na kura moja.”

Mbali na hayo Ruhinda alisema zoezi la kuchukua fomu na kurudisha fomu za maombi katika ngazi ya Kila Wilaya na Mkoa litaanzaa aaa 2 kamili asubuhi na kumalizika saa 9 kamili alasiri ambapo fomu ya maombi ya kugombea nafasi ya baraza itatolewa Bure na Msimamizi wa uchaguzi.

Aliongeza kuwa mgombea atakosa sifa ya kupigiwa kura endapo maombi yake yatabainika kutokujaza fomu za maombi kwa usahihi na ukamilifu, kutokuwa na vitambulisho vinavyotakiwa kwa mujibu wa kanuni na uchaguzi lakini pia kutokuwa na sifa za msingi zilizoainishwa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi

Kwa upande wa kampeni za kupiga kura Ruhinda alisema wagombea watanadi sera zao kwa wapiga kura katika kila mkutano wa uchaguzi na zoezi la upigaji kura litafanyika kwa Siri.

Pia alisema “Wapiga kura ni wawakilishi wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali yaliyokidhi vigezo, Wagombea wataonesha barua ya uthibitisho kutoka Mashirika yasiyo ya Kiserikali wanayowakilisha na nakata ya cheti cha usajili, Wagombea katika ngazi ya mkoa ni wawakilishi watatu (03) waliochaguliwa katika ngazi ya Wilaya, Wagombea katika ngazi ya Taifa ni wawakilishi wa Baraza waliochaguliwa katika kila mkoa wakiwemo Mashirika yasiyo ya Kiserikali ya Kimataifa na Makundi Maalum, Uchaguzi wa Makundi Maalum utahusisha Mwakilishi wa Mashirika ya Kimataifa na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanayotekeleza alua za Watu Wenye Ulemavu, Vijana na Watoto)”

Kuhusu uhesabuji Kura na Kutangaza Matokeo Ruhinda alisema Kura zitahesabiwa baada ya upigaji kura kumalizika katika ngazi husika na zitahesabiwa chini ya Msimamizi wa Uchaguzi na Mwangalizi wa Uchaguzi.

Pia alisema Kila mgombea atakuwa na mwakilishi wake atakayehakiki kura za mgombea wake na Mgombea ataandika maelezo na kuyawasilisha kwa Msimamizi wa Uchaguzi ikiwa hajaridhia matokeo.

Ruhinda aliongeza kuwa “Msimamizi wa Uchaguzi atatangaza matokeo mbele ya wapiga kura/wagombea Msimamizi, wa Uchaguzi atatangaza matokeo kwa kuanza na mgombea mwenye kura ndogo, Wagombea watatu (03) wenye kura nyingi zaidi ya wengine ndiyo watakuwa washindi katika ngazi ya Wilaya lakini pia mgombea mwenye kura nyingi zaidi ya wengine ndiye atakuwa mshindi katika ngazi ya Mkoa. Vivyo hivyo, Mgombea mwenye kura nyingi zaidi ya wengine ndiye atakuwa mshindi katika uwakilishi wa Makundi Maalum, uwakilishi wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali ya Kimataifa na katika nafasi za uongozi wa ngazi ya Taifa.”