Na. Israel Mwaisaka, TimesMajira Online, Rukwa
Wananchi wa mwambao wa Ziwa Tanganyika mkoani Rukwa wametakiwa kuwa na vyoo bora na kuhakikisha kila kaya na jamii inajenga utamaduni wa kutumia vyoo ili kujikinga na ugonjwa wa kipindupindu.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga amebainisha hayo leo (Desemba 01,2022) katika kijiji cha Kamwanda Kata ya Kirando Wilaya ya Nkasi wakati akihutubia kwenye maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani ambapo alisema hafurahishwi kuona ugonjwa wa kipindupindu ukiripotiwa maeneo hayo.
“Wilaya hii ya Nkasi inaongoza kwa kusambaa ugonjwa wa kipindupindu kwa sababu za watu kutotumia vyoo. Mkuu wa Wilaya na Kamati ya Usalama nataka mfanye kazi ya kusimamia zoezi la uwepo vyoo bora na safi katika ukanda wa ziwa Tanganyika .Sitaki mwaka huu kusikia ripoti za kipindupindu Kirando” alisema Sendiga.
Maeneo ya mwambao wa Ziwa Tanganyika katika wilaya za Nkasi na Kalambo kwa nyakati mbalimbali yamekuwa na matukio ya mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu hususan wakati wa mvua za masika ambapo sababu kubwa imeleezwa wakazi wake kutokutumia vyoo safi na bora.
Kuhusu mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi ,lSendiga alisema serikali itaendelea kuhakiksha wananchi wote walio na maambukizi wanapata dawa za kufubaza virusi kwenye vituo vyote vya afya na kuwa watalaam wataendelea kutoa elimu ili kudhibiti maambukizi mapya.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa wa Rukwa alizindua kampeni ya utoaji chanjo ya polio awamu ya nne iliyoanza leo ambapo mkoa huo umelenga kuwafikia watoto zaidi ya 360,000 katika siku nne za kampeni.
Naye mratibu wa maaadhimisho ya Siku ya UKIMWI mkoani Rukwa Aziza Kalyatila alisema maambukizi yamepungua toka asilimia 6.2 mwaka 2015/16 hadi asilimia 4.4 mwaka 2016/2017 ambapo kundi lililohatarishi kupata maambukizi mapya ni la watu wenye umri kati ya miaka 25 hadi 49.
Akitoa salamu za wananchi wa Nkasi , Mkuu wa Wilaya hiyo Peter Lijualikali alisema maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani yamelenga kuwakumbusha jamii kuwa ugonjwa wa Ukimwi bado upo hivyo jamii ichukue tahadhali na kufuata ushauri wa watalaam wa afya.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato