June 13, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kipanga azindua kituo cha Mawasiliano,Serikali yaahidi elimu bora kwa Wote

Na Joyce Kasiki, Dodoma

NAIBU Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,  Omary Juma Kipanga amezindua rasmi Kituo cha Mawasiliano cha Wizara hiyo kilichopo katika Mji wa Serikali, Mtumba  mkoani  Dodoma.

Akizindua kituo hicho Jana Mtumba jijini Dodoma Kipanga alisema,tukio hilo  ni sehemu ya mageuzi ya kijamii na kielimu yanayoendelea chini ya serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Katika hotuba yake ya uzinduzi,  Kipanga aliwashukuru kwa dhati washirika wa maendeleo, hususan Serikali ya Uingereza kupitia ofisi ya FCDO, kwa kusaidia kuboresha kituo cha zamani cha simu kuwa kituo kamili cha mawasiliano kupitia mradi wa Shule Bora. 

“Kituo hiki ni ushahidi mwingine wa dhamira ya dhati ya Serikali ya Uingereza kusaidia elimu nchini kwa lengo la kuwa na taifa lenye ujuzi na maarifa kwa maendeleo endelevu,” alisema Kipanga

Alisema,mradi wa Shule Bora una thamani ya pauni milioni 89 sawa na takribani shilingi bilioni 271 za Kitanzania, na unatarajiwa kutekelezwa kwa kipindi cha miaka sita kuanzia mwaka 2021 hadi 2028. Mradi huu unalenga kuboresha ubora wa elimu, usawa wa kijinsia, na mazingira salama ya kujifunzia kwa watoto wa kike na wa kiume katika mikoa tisa ya Tanzania, ikiwa ni pamoja na Dodoma, Tanga, Simiyu na Katavi.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, Kituo hicho kitakuwa msaada mkubwa wakati huu ambapo Wizara iko katika utekelezaji wa Sera mpya ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, Toleo la 2023, ambayo ilizinduliwa rasmi tarehe 1 Februari 2025 na Rais Samia. 

Alisema Sera hiyo inalenga kuandaa vijana kwa ajili ya ajira kupitia mfumo wa elimu ya msingi wa lazima wa miaka 10 na mwelekeo mpya wa elimu ya kiufundi na ya jumla kwa shule za sekondari.

Akifafanua zaidi, Naibu Waziri alisema kuwa kituo hiki hakitakuwa tu kwa ajili ya kupokea simu, bali ni daraja la mawasiliano linaloimarisha uwazi, uwajibikaji na ushiriki wa wananchi katika mageuzi ya elimu.

 “Hiki si kituo cha kawaida, bali ni ishara ya utawala jumuishi na uwazi katika sekta ya elimu nchini,” alisisitiza.

Serikali pia imetoa shukrani kwa kampuni ya Flex Corporate Services Ltd iliyotoa usaidizi wa kitaalamu katika tathmini, ushauri wa kiteknolojia na mafunzo kwa watumishi wa Wizara, hatua ambayo imehakikisha kituo hiki kinafanya kazi kwa ufanisi mkubwa. Kampuni hiyo ilisaidia kuamua teknolojia sahihi ya vifaa vya mawasiliano pamoja na mfumo wa kuendesha kituo hicho.

 Kipanga aliwataka wafanyakazi wa kituo hicho kipya kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi, ubunifu na kwa kuwahudumia wananchi kwa moyo wa kizalendo. 

“Nyuma ya kila simu au ujumbe unaopokewa, kuna mwanafunzi ambaye mustakabali wake unategemea taarifa au msaada wetu,” alikumbusha kwa msisitizo.

 Naibu Waziri alisema, matumaini yake kuwa kituo hicho kitatumika kikamilifu kwa lengo la kuongeza ushiriki wa wadau katika mageuzi ya elimu, huku akiahidi kuwa Wizara itaendelea kushirikiana na wadau wote katika kuhakikisha elimu bora inapatikana kwa kila mtoto hapa nchini bila kumwacha yeyote nyuma.

Awali ,Katibu Mkuu Wizara ya Elimu ,Sayansi na Teknolojia Prof.Carolyne Nombo ameishukuru Taasisi ya FDO kupitia mradi wake wa shule Bora  ambao wameshiriki katika kupatikana kituo hicho ambacho alisema  kitakuwa chachu katika kuboresha utendaji kazi wa watumishi wa Wizara hiyo.

Aidha alisema  kituo hicho linakwenda kuboresha mawasiliano kati ya Wizara hiyo na Wadau wake na kuwafikia mahali waliopo.

“Kwa hiyo kwa ujumla kituo hiki kitakuwa ni njia ya kuwaelimisha watanzania juu ya mabadiliko makubwa katika sekta ya Elimu.