Na Moses Ng’wat, Timesmajira Online,Songwe
WAHITIMU wa Taasisi ya Teknolojia Dar es salaam (DIT) kampasi ya Myunga iliyopo wilayani Momba, Mkoa wa Songwe, wametakiwa kutumia hazina kubwa ya elimu ya ufundi waliyoipata kwa manufaa ya Taifa.
Rai hiyo imetolewa Januari 10, 2024 na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga, aliyemuwakilisha Waziri wa Wizara hiyo, Prof. Adolf Mkenda, kwenye mahafali ya 17 duru ya tatu (DIT) Kampasi ya Myunga, yaliyofanyika chuoni hapo.
Amewataka kutambua kuwa elimu waliyoipata ni matunda ya kujinyima kwa wazazi na walezi wao, ikiwemo dhamira ya serikali ya kuendelea kuongeza fursa za mafunzo ya ufundi na kusimamia ubora wa elimu ili kuwezesha taifa kuwa na rasilimali watu wanaokwenda kuwa chachu.
“Hakika haya ni matunda ya kujinyima kwa wazazi na walezi wenu, sasa mkiwa wahitimu bila shaka mnatambua hazina kubwa ya elimu ya ufundi mliyopata, ni imani yangu mtaitumia kwa manufaa yenu binafsi, familia zenu na Taifa letu kwa ujumla,” ameeleza Kipanga.
Aidha amesema kuwa katika kugharamia elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, serikali imewezesha huduma ya chakula kwa wanafunzi 18,723 katika vyuo vya maendeleo ya wananchi (FDC), chuo cha ufundi Arusha,Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya(MUST) pamoja na DIT.
Awali, Mwenyekiti wa Baraza la Taasisi ya Teknolojia Dar es salaam (DIT), Mhandisi Daktari Richard Masika, ameeleza kuwa serikali kwa kuipatia taasisi hiyo imetoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ukiwemo mradi wa Technica Education and Labour Market Support Project (TELMS II) ambao unatekelezwa kwa fedha za mkopo wa riba nafuu wa bilioni 34 kutoka serikali ya Italia.
Daktari Masika amesema sehemu ya fedha hizo kiasi cha bilioni 3.5 zitatumika katika Kampasi ya Myunga kwa ajili ya kujenga jengo la ghorofa nne litakalokuwa na uwezo wa kutumiwa na wanafunzi 1000 kwa wakati mmoja.
Katika mahafali hiyo jumla ya wahitimu 13 kati ya hao sita wakiwa ni wa kike na saba wa kiume walitunukiwa cheti cha taifa cha ufundi stadi ngazi ya pili (National Vocation award level II) katika fani ya ufundi bomba, huku wahitimu wanne wa nyongeza nao walitunikiwa shahada na stashahada katika fani za uhandisi wa ujenzi.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa