January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kiongozi wa Mwenge ahimiza umakini utekelezaji wa miradi

Na Cresensia Kapinga, TimesMajira,OnlineSongea

KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Sahili Nyanzabara Geraluma amewataka wahandisi kuacha kufanya kazi kwa woga kwa sababu ya Mwenge unapita katika maeneo ya miradi yao badala yake wafanye kazi kwa umakini ili majengo yanayojengwa yawe bora na si vinginevyo.

Hayo aliyasema jana wakati akiweka jiwe la msingi kwenye eneo la viwanda iliyopo Mtaa wa Lilambo B Kata ya Lilambo Manispaa ya Songea.

Amesema majengo yanayojengwa kwa fedha za Serikali ni lazima yahakikishe yanasimamiwa hatua kwa hatua sio yanajengwa kwa kulipua lipua kisa uoga wa Mwenge unapita.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Sahili Nyanzabara Geraluma akifungua mradi wa viwanda uliopo Manispaa ya Songea Mtaa wa Lilambo B Kata ya Lilambo Manispaa ya Songea.

“Viwanda hivi vitasaidia kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja pia uchumi wa taifa letu, akina mama nanyi mjiunge kwenye vikundi kwa ajili ya kukopa pesa sio mnakaa tu na kulilia maisha magumu wakati Manispaa kuna pesa hamzichukui na hamzitumii.” Amesema Geraluma.

Mkuu wa Wilaya ya Songea, Pololet Mgema akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Sahili Nyanzabara Geraluma. Mwenge huo utakimbizwa katika Manispaa ya Songea ikiwa ni pamoja na kukagua kuweka jiwe la msingi na kufungua miradi yenye thamani ya sh. Bilioni 1.4.

Aidha amesema ni lazima wananchi wanufaike na mapato ya fedha za ndani za Halmashauri lakini pia wahakikishe wanasimamia miradi inayotekelezwa kila hatu kwani mwisho wa siku majengo hayo yanabaki kuwa yao.