December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa aridhishwa na mradi wa barabara Ilemela

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa mwaka 2023 Abdallah Shaib Kaim,ameridhishwa na mradi wa barabara za mitaa ya Kirumba( Magomeni na Kabuhoro) iliopo Kata ya Kirumba wilayani Ilemela zenye urefu wa kilomita 0.9 na thamani ya zaidi ya milioni 998.2.

Akizungumza wakati akizindua barabara hiyo Kiongozi huyo wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa ameeleza kuwa mradi huo umekidhi vigezo na umeendana na thamani ya fedha iliyotolewa.

Awali akisoma taarifa ya mradi huo Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Ilemela Mhandisi Sobe Makonyo, ameeleza kuwa mradi wa ujenzi wa barabara za mitaa ya Kirumba (Magomeni, Kabuhoro hadi ziwani) ni kati ya miradi ambayo inatekelezwa na tozo ya mafuta kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Mhandisi Sobe ameeleza kuwa barabara ya Magomeni inaanzia Mwaloni hadi Kabuhoro na nyingine inaunga Penda hadi Kabuhoro(Magengeni) ambapo mradi ulianza kutekelezwa Januari mwaka huu na kukamilika Julai 2023.

Amesema mradi huo una gharama ya zaidi ya milioni 998.2 na umetekelezwa na Mkandarasi Nyanza Roads Works,umejengwa kwa kiwango cha lami nzito.

Huku kazi zilizotekelezwa katika mradi huo ni ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa Km 0.6,kutoka Mwaloni hadi Kabuhoro,ujenzi wa barabara kiwango cha lami Km 0.3,kutoka makutano ya Penda(Penda Junction) hadi Kabuhoro Magengeni na kuweka taa za barabarani Km 0.9.

“Mchanganuo wa gharama za kazi zilizofanyika ni maandalizi ya awali zaidi ya milioni 61,barabara ya Magomeni zaidi ya milioni 612 na barabara ya Kabuhoro hadi ziwani zaidi ya milioni 323,”amesema Mhandisi Sobe.

Pia ameeleza kuwa mradi huo utarahisisha huduma ya usafiri kwa wananchi,kuvutia biashara na uwekezaji hatimaye kuongeza pato la taifa,kuongeza kasi ya uwekezaji kwenye mwambao wa Ziwa Victoria pamoja na kuongeza kasi ya ukuaji wa Jiji la Mwanza.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt.Angeline Mabula ameeleza kuwa kabla ya barabara hiyo wananchi wa maeneo hayo walikuwa wanapata shida endapo watapata msiba namna ya kusafirishwa maiti kwenda kuzika ilikuwa shida au kumpeleka mgonjwa hospitali.

Dkt.Angeline ameeleza kuwa kipande kilicho baki cha barabara ambacho ni eneo la mlima watajenga barabara kwa kiwango cha zege.

Sanjari na hayo ameshukuru Rais Samia kwa kuendelea kutoa fedha ambapo Jimbo hilo limepata fedha ya kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo afya, elimu pamoja na barabara.

Mwenge wa Uhuru umekimbizwa katika Kata 6 kati ya 19 za Wilaya ya Ilemela kwa umbali wa km 57 ambapo jumla ya miradi 4 na shughuli 7 zenye thamani ya zaidi bilioni 1.3 zimetembelewa.