Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Lushoto
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2024 Godfrey Mnzava amewahskikishia wananchi wa Kitongoji cha Magamba Cost Juu Kata ya Magamba, Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga kuwa watapata maji.
Ni baada ya kupokea malalamiko ya wananchi hao kupitia viongozi wa Wilaya ya Lushoto kuwa mradi wa maji Magamba- Lushoto Mjini umewatenga wakati chanzo cha maji kinatoka kwenye kata yao.
Ameyasema hayo Aprili 12, 2024 wakati alipotembelea na kukagua mradi huo, ambao utanufaisha wananchi zaidi ya 30,000 kwenye Mji wa Lushoto na viunga vyake.
Ili kuwathibitishia kuwa na wao watapata maji, Mnzava amezungumza kwa njia ya simu na Waziri wa Maji Jumaa Aweso huku wananchi wakisikiliza ambapo Waziri huyo ametoa maelekezo kwa watumishi wa sekta ya Maji Mkoa wa Tanga kufanyia kazi suala hilo.
“Waziri,wananchi wa Kitongoji cha Magamba Cost Juu wameona hawapo kwenye coverage ya mradi huu wakati wameona Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kwa ajili ya mradi huu, Mama ametoa bilioni 1.8, lakini wao wanaelezwa hawamo kwenye utekelezaji wa mradi huu, sasa unawaeleza nini kwenye hili,” amesema Mnzava.
Waziri aweso amesema tayari ameshatoa maagizo kwa viongozi akiwemo Meneja wa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo kukaa Aprili 22, mwaka huu na Mkandarasi ataekaejenga mradi wa peke yao wananchi wa Magamba Cost Juu, na zaidi ya sh. milioni 300 zimetengwa kwa shughuli hiyo.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Lushoto, Mdathiru Adinan amemueleza Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kuwa tayari mkataba wa kujenga visima kwa wananchi wa Magamba Cost Juu umeshasainiwa wakati wowote mkandarasi ataanza kazi ndani ya mwezi huu wa Aprili.
Akisoma taarifa ya mradi huo, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Lushoto Mhandisi Erwin Sizinga amesema ujenzi wa miundombinu ya mradi huo ni
miongoni mwa miradi ya maji inayoendelea kutekelezwa na ofisi yake kupitia fedha za Mfuko wa Taifa wa Maji, na mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi M/S PNR Services Ltd wa Dar es Salaam.
Mkataba huo ulianza Novemba 17, 2022, na unategemea kukamilika Juni 30, 2024, ambapo mradi huo utakapokamilika utatoa lita 1,950,000 unatarajiwa kuhudumia wananchi 30,835 wanaoishi maeneo ya Magamba.
Huku maeneo mengine yatakayohudumiwa na mradi huo ni Kwesimu, Bara, Jegestal, Kambi namba nne, Chakechake, Kitivo, Maguzoni,Sinza, Lushoto Mjini, Mabwawani, Kipembe na Kialilo.
“Kazi zilizofanyika ni pamoja na ujenzi wa chanzo kipya cha maji eneo la Kibohelo utekelezaji wake umefikia asilimia 95, uchimbaji wa mitaro distribution line urefu wa mita 14,600 asilimia 100, uchimbaji wa mitaro Gravity main urefu wa mita 5,400 asilimia 40, uunganishaji na ulazaji wa bomba asilimia 80, na ujenzi wa chemba za airvalve na washout asilimia 50,”ameeleza na kuongeza kuwa:
“Gharama za mradi ni bilioni 1.8, mpaka sasa Mkandarasi ameshalipwa milioni 647.37 sawa na asilimia 35.9 ya fedha yote ya mradi ambao upo asilimia 75,”amesema Mhandisi Sizinga.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba