Na Judith Ferdinand,TimesMajira Online,Mwanza
KIONGOZI wa mbio maalumu za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2021 Luteni Josephine Mwambashi ameridhishwa na matumizi ya fedha katika mradi wa huduma ya maji kwa jamii.
Mradi huo uliopo Majengo Mapya Nyegezi Wilayani Nyamagana mkoani Mwanza uliotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA).
Luteni Mwambashi amebainisha hayo jana wakati akiweka jiwe la msingi katika mradi huo,ambapo amesema alikuwa anaangalia nyaraka ameona kwamba fedha kweli zimesimamiwa vizuri lakini pia amepanda kwenye tenki juu na ameona maji yapo.
Amesema,chanzo kikubwa ni Ziwa Victoria ambalo linaingiza maji kwenye tenki hilo kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi,lakini maji yapo na baadhi ya wananchi wameisha unganishiwa huduma hiyo na wanapata maji.
“Ndugu zangu tupo hapa kwenye mradi wa maji,nafahamu umeisha anza kutoa huduma ya maji,kwa baadhi ya wananchi kwa sababu mradi huu unahusisha sana kuwaunganisha maji wananchi moja kwa moja katika makazi yao,”amesema Luteni Mwambashi.
Pia amesema,ilitokea changamoto kidogo kwa baadhi ya wananchi kuto unganishiwa maji kutokana na kukosekana kwa mita kwa sababu ya COVID-19 ambapo mita zinaagizwa nje ya nchi lakini taarifa alioipata hapo ni kwamba mita zimekwisha fika na fomu za watu walizoomba kwa ajili ya kuunganishiwa maji zipo tayari.
Hivyo zoezi la kuunganishiwa maji litaanza mara moja ili wananchi wote waweze kupata huduma hiyo ya maji ambapo aliwaomba wananchi kuwavumilia wataalamu wa maji kwa sababu walipata changamoto hiyo.
“Mkuu wa Wilaya kama ulivyoniahidi kuwa umeziona fomu na umezisaini tayari kwa ajili ya kuanza zoezi la kuingiza maji kwa wananchi ambao hawajapata,kwa sababu mita zimeisha fika kwaio zoezi hilo lifanyike watu wapate maji ambayo ni uhai na msingi sana kwa wananchi,” amesema Luteni Mwambashi na kuongeza kuwa.
“Wananchi wakiona tenki kubwa namna hii na lipo karibu halafu hawapati maji inakuwa ni changamoto lakini ndugu zangu tunafahamu wakazi wa Mwanza kuwa tupo wengi na tenki hili lina hudumia watu wengi kwaio maji haya yanakuwa ya mgao kutokana na mahitaji mengi ya wananchi,ni sisitize kwamba zoezi lianze na kuwahudumia wale ambao fomu zao zimeisha kamilika,” amesema.
Akisoma taarifa ya mradi huo kwa Luteni Mwambashi kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA Mhandisi Leonard Msenyele,Meneja Miradi wa mamlaka hiyo Mhandisi Gogadi Mgwatu amesema, utekelezaji wa mradi umekamilika kwa asilimia 100 na utawanufaisha wananchi 10,500 kutoka Kata za Nyegezi,Mkolani na Buhongwa wilayani Nyamagana.
Mhandisi Mgwatu amesema,mradi huo wenye thamani ya zaidi ya bilioni 3.7,fedha kutoka serikali kuu na wahisani wa Benki ya uwekezaji ya Ulaya(EBI) na taasisi ya watu wa Ufaransa (AFD),una tenki lenye ujazo wa lita milioni 1.2 na urefu wa mita 3,778.
More Stories
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi
Rais Samia apongezwa kwa kuboresha huduma kwa wazee
Watu 5,000 kuhudhuria tamasha la utamaduni Songea