December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwenge waridhishwa na miundombinu ya maji

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Korogwe

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2024 Godfrey Mnzava ameridhia uboreshwaji wa miundombinu ya maji katika Mji wa Korogwe uendelee .

Mnzava amesema mapungufu ya ndani yaliyojitokeza yatashughulikiwa na utawala wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Korogwe William Mwakilema, lakini kwa ujenzi wa mradi kuanzia kwenye chanzo (dakio), tenki la maji hadi sehemu ya kusambaza maji, hivyo vyote vimejengwa kwa weledi mkubwa.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Godfrey Mnzava akiangalia bomba la usambazaji maji likitoa maji

Ameyasema hayo Aprili 10, 2024 alipotembelea na kukagua ujenzi wa mradi wa uboreshaji wa upatikanaji wa maji katika Mji wa Korogwe na viunga vyake ambapo alifika Kata ya Mtonga kwa ajili ya kuangalia bomba la usambazaji maji.

“Mwenge wa Uhuru kwa kuzingatia maslahi mapana ya wananchi wa Mji wa Korogwe kupata huduma ya maji kama ambavyo imekuwa dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kwamba mama anatuliwa ndoo kichwani, na kuondokana na mateso na masumbuko ambayo walikuwa nayo kwa muda mrefu ya kukosa maji safi, salama na yenye uhakika,”amesema Mnzava na kuongeza:

“Kwa kulizingatia hilo Mkuu wa Wilaya hasa baada ya kukagua kwenye chanzo, storage tank (tangi la kuhifadhi maji), na hapa ambapo usambazaji wa maji umefanyika na kuridhika kazi hizo zimefanyika, na uhakika wa maji wananchi wataendelea kuupata, yale mengine yaendelee kufanyika kama tulivyoelekezana, Mwenge wa Uhuru upo tayari kufungua maji pale ili wananchi waendelee kupata huduma ya maji,” amesema Mnzava.

Akisoma taarifa ya mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira wa HTM Mhandisi Yohana Mgaza amesema mradi wa uboreshaji miundombinu ya maji katika Mji wa Korogwe unatekelezwa na Mkandarasi Frangem International LTD na kusimamiwa na wataalam wa HTM.

Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo akizungumza na wananchi wa Kata ya Mtonga, Korogwe Mjini

Mhandisi Mgaza amesema mradi ulianza kutekelezwa rasmi Agosti 11, 2022 na ulitarajiwa kukamilika Machi 17, 2023, lakini kutokana na changamoto za upatikanaji wa fedha kwa wakati haujakamilika kwa muda uliopangwa na badala yake unategemewa kukamilika Mei 6, 2024.

Ambapo ameeleza lengo la mradi huo ni kuongeza uzalishaji wa maji na kukarabati miundombinu ili kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji Korogwe Mjini.

“Mradi huu unategemewa kugharimu kiasi cha bilioni 1.5 kutoka Serikali Kuu hadi sasa umefikia asilimia 95,tayari unatoa huduma kwa wananchi ambapo jumla ya bilioni 1.3 zimepokelewa na kutekeleza ujenzi wa kidakio cha maji cha Mashindei, kulaza bomba hadi kwenye tenki la Kwamkole kilomita 12.56, ujenzi wa Break Pressure Tank 5 na ukarabati wa miundombinu ya maji katikati ya Mji kilomita 12.6,”.

Mkurugenzi Mtendaji wa HTM Mhandisi Yohana Mgaza akisoma taarifa ya mradi

Pia ameeleza kuwa ili kukamilisha utekelezaji wa mradi kinahitajika kiasi cha milioni 194.3 kwa ajili ya ununuzi na ulazaji wa mabomba na viungio vyake kilomita 24.9.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Godfrey Mnzava akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa HTM Mhandisi Yohana Mgaza kuhusu muundo wa ujenzi wa mradi wa uboreshaji wa miundombinu ya maji