Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline, Dodoma
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana amewaomba Watanzania kutokubali hoja za kejeli, chuki na kufarakanisha watu ambazo zimekuwa zikitolewa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Amesema viongozi wa CHADEMA kwa nyakati tofauti katika mikutano yao ya hadhara wamekuwa wakieneza chuki, uongo na kuzusha kauli za uchoganishi dhidi ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa hoja dhaifu kwamba anatoka Zanzibar.
Akizungumza jana jijini Dodoma mbele ya viongozi, wana CCM pamoja na wananchi wakati wa mkutano maalumu wa CCM Mkoa wa Dodoma, Kinana alisema CHADEMA imepata uhuru mkubwa kufanya maandamano, mikutano ya hadhara, kuzunguka sehemu mbalimbali
“Katika mizunguko yao CHADEMA wamesema mengi, wametutuhumu CCM, serikali, wamemtuhumu Rais kwa mambo ya uongo. Hatukatai kukoselewa, hatukatai kusahihishwa, lakini hatukubali kuzuliwa au kushutumiwa kwa mambo ambayo hayapo.
“Kubwa ambalo wamefanya ni kujenga chuki miongoni mwa Watanzania, kujenga mifarafakano. Wakaenda mbali zadi wakaanza kuzusha jambo ambalo wanataka kuifanya ajenda, wanasema nchi ina Rais ambaye ni Mzanzibari na anaihujumu Bara, lakini ajenda hiyo imeshindwa,” alisema.
Akifafanua zaidi alisema CHADEMA wanazungumza kuhusu Rais Samia ni Mzanzibar, hana huruma na Bara, hana jema analofanya kwa Bara, hana msaada.
“Wanataka kumtenganisha Rais na Watanzania, nani amekataa kwamba Rais Samia sio Mzanzibari. Ni Mzanzibari na ametokana na Katiba ambayo inaeleza mgombea urais akitoka Zanzibar basi mgombea mwenza anatoka upande wa pili
Ndivyo tulivyokubaliana na huyu ni mgombea mwenza ana nafasi sawa na mgombea urais. Ikitokea mgombea mwenza hayuko uchaguzi unaahirishwa. Mwaka 2005 uchaguzi uliahirishwa kwa sababu mgombea mwenza wa CHADEMA alifariki dunia.
“Halafu leo wanakejeli kiongozi kutoka Zanzibar, wametafuta namna ya kushughulika na Rais (Dk. Samia) lakini wakiangalia barabara zinajengwa, bwawa la mwalimu Nyerere limefika pazuri, ujenzi wa mji wa Dodoma unaendelea kwa kasi.
“Reli ya mwendo kasi sasa imefika Dodoma na ujenzi unaendelea sasa wanakosa hoja wanakuja na maneno ya kuzusha kwamba Rais hafai kwa sababu anatoka Zanzibar. Rais Samia ni Rais wa katiba amechukua uongozi baada ya Rais Dk. John Magufuli kufariki dunia,” alisema.
Ameogeza “Rais Samia alikuwa Mgombea Mwenza akawa Makamu wa Rais, na awamu ya pili Magufuli akamteua tena lakini oooh… huyo Mzanzibar ili watu baadae polepole waanze kusema tunatawaliwa na Mzanzibari.”
Kinana amewaomba Watanzania kupuuza uzushi huo na kushauri wasimame na Rais Samia kwani anafanya kazi nzuri. Tangu awamu mbalimbali zilizopita kuna sera iliyoanza baada ya Mzee Mwinyi (Hayati Rais mstaafu) kuchukua nchi kwa kuanzisha sera ya sekta binafsi kushiriki kukuza uchumi.
“Leo CHADEMA wanasema Rais Samia anauza kila kitu, kauza nini?. Awamu ya Tatu Rais mstaafu Benjamin Mkapa alibinafsisha mashirika zaidi ya 200 kwani alikuwa Mzanzibar? Lakini alifanya hivyo kwa maslahi ya Taifa.
“Wakati TICS wanapewa bandari ya Dar es Salaam nchi haikuuzwa, lakini baada ya kupewa DP World nchi inauzwa. Hivi mnaamini kweli Rais anaweza kukaa na kufanya jambo ambalo halina nia njema na nchi yetu.
“Rais haamui peke yake kuna vyombo ambavyo vinakaa na kuangalia mambo na kisha vinamshauri Rais. Kataeni juhudi zinazofanyika za kujenga chuki dhidi ya Rais. Kuna wakati Shirika la Reli Tanzania (TRC) lilikabidhiwa kwa RITES (kampuni) kutoka India? Alikabidhi Rais Samia?”
Kinana alisema hayo mambo yanafanyika kwa malengo na hasa kuleta tija na ufanisi, hivyo Watanzania wasikubali kusikiliza hoja rejareja, hoja za msimu.
“Wanakwenda wanakaa katika kiwanda cha kutengeneza uongo na uzushi na kisha wanaanza kuituhumu CCM na serikali yake. Hatukatai kukoselewa, hata Rais Samia hakatai, sisi si malaika tunakosea. Tunasahihishwa, lakini kudharauliwa na kutukanwa hapana.
More Stories
Balozi Nchimbi kuongoza waombolezaji mazishi ya Kibiti leo
Dkt.Tulia,apewa tano kuwezesha wananchi
Nkasi yajipanga kukusanya mapato