November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kinana ahaidi kusimamia haki kuifanya  CCM kuwa imara Kidemokrasia

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

WAJUMBE 1875 wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi(CCM),Taifa wamepiga kura ya kumuidhinisha Mgombea wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho ambapo Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM,Abdulrahman Kinana ameshinda kiti hicho kwa kura zote zilizopigwa na wajumbe hao ambazo ni sawa na asilimia 100.

Kura hizo zimepigwa jijini hapa leo kwenye Mkutano Mkuu  wa CCM na baada ya kushinda kiti hicho Kinana amemshukuru
Mwenyekiti wa Chama hicho Samia Suluhu Hassan,ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku akihaidi kwenda kusimamia Chama kuwa imara Kidemokrasia na kusimamia haki ya kuchaguliwa bila upendeleo.

Ambapo ametaja baadhi ya haki atakazo enda kusimamia ni pamoja na haki ya mwana chama kutoa Mawazo.

“Lazima wanachama wawe Huru kutoa mawazo, hakuna mwenye hakimiliki ya mawazo, lazima tumsikilize kila mwananchi, na wanachama wakimchagua mtu kwani sisi ni nani wa kupinga”amesema.

“Juzi uliniita nikawa najiuliza nimeitiwa nini, nikajua ni katika kusalimiana lakini Rais akaniambia nataka uwe Makamu Mwenyekiti, nikamwambia sina hiari, sina budi kukubali, napenda kukuhakikishia Mwenyekiti nitajitahidi kadri ya uwezo wangu kufikia matarajio yako na niseme sitokuangusha”amesema

Pia ameishukuru Kamati Kuu kwa kupitisha jina lake, pamoja na wajumbe wa Halmashauri kuu kwa kupitisha na kuidhinisha jina lake na kusema wamempa  imani kubwa, na yeye atakitumikia Chama chake,wana CCM na Watanzania kwa ujumla.

Hata hivyo amemshukuru aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Philip Mangula ambapo amesema amejifunza mengi kutoka kwake na kumpongeza kwa kustaafu kwa Heshima

“Kama Mangula asingeamua kustaafu, basi leo nisingekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi”amesema.

Makamu Mwenyekiti Kinana aliwashukuru Wenyekiti wote kuanzia Baba wa Taifa mpaka sasa Rais Samia Suluhu Hassan na kusema kuwa mengine ni mapungufu yake mwenyewe.

Ameeleza kuwa CCM si mali ya Serikali ila Serikali zinatokana na CCM ambapo ameeleza kuwa CCM haipokei maelekezo kutoka Serikalini bali Serikali inapokea maelekezo toka CCM.

“CCM haiagizwi na Serikali, CCM inaagiza Serikali, na wanaokwenda kuomba kura ni CCM sio Serikali, niwasihi Viongozi wetu msitudhurumu hiyo haki”ameaisitiza.

“Serikali inapokuwa na mapungufu wenye jukumu la kuzisemea kasoro ni Chama na hatutazisemea kwa kukejeli, tutaitana kwenye Vikao vyetu vya ndani, si sawa kwa Mwana CCM kwenda hadharani kuisema vibaya Serikali yake”amesema.