January 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kilongawima yajipanga kuimarisha ulinzi na usalama

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online, Dar

SERIKALI ya Mtaa ya Kilongawima iliyopo Kata ya Kudunchi Wilaya ya Kinondoni imejipanga kuimarisha ulinzi na Usalama katika kata hiyo kwa kufuata agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Amos Makalla alilolitoa hivi karibuni baada ya kutokea mauaji ya Mtendaji wa Kata Msuvi Manispaa ya Ubungo kuuwa na watu wasiojulikana.

Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki Mwenyekiti wa mtaa wa Kilongawima Emmanuel Mkuchu amesema maelekezo yote yaliotolewa na RC huyo yanatekelezwa kwa wakati yeye kama kiongozi wa ulinzi na usalama katika Mtaa huo kwa kushirikiana na viongozi wenzake.

Amesema kata hiyo itadumisha ulinzi zaidi kwa wananchi na katika Ofisi za kata hiyo ili kuweza kudhibiti chagamoto ya uvamizi wa watu wasiojulikana na wenye nia mbaya .

“Kwa sasa hali ya usalama katika kata yetu ni nzuri kwa hali matukio mbalimbali yaliokuwa yakitolewa awali yamezidi kupungua hivyo kama mtaa tumejipanga kuimarisha zaidi ulinzi Kama njia ya kuyafanyia kazi maagizo yaliotolewa na mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Amos Makalla”amesema Mkuchu.

Mwenyekiti wa mtaa wa Kilongawima Emmanuel Mkuchu

Akizungumza kuhusu miradi ya mbalimbali katika Kata hiyo Mkuchi amesema kwa upande wa maendeleo katika bajeti ya Halmashauri ya Serikali iliyopita wameweza kufaidika katika upande wa miundombinu ikiwemo Barabara zaidi ya mbili hadi tatu ambazo zimeweza kuingizwa na kufanyiwa marekebisho.

Akitaja barabara hizo ni pamoja na Barabara ya Jagwani, Maliasili ambazo katika kipindi hiki zitakwenda kuwa salama na safi.

Pia amesema walikuwa wakikabiliana na chagamoto ya wakazi wa Maliasili kufugiwa njia ambalo mkuu wa wilaya ya Kinondoni tayari amefika na kuweza kulitafutia ufumbuzi zaidi .

Ameongeza kuwa, katika ofisi ya mtaa wa kilongawima wanabustani ya Serikali ambayo ipo chini ya halmshauri inayojulikana kama butaniki garden tayari imetengewa bajeti ya Millioni 500 kwa ajili ya kuiendeleza, sambamba na kuboresha Viwanja vya michezo. .

“Kukamlika kwa bustani hii kutakuwa kivutio kikubwa kwa wakazi na kuweza kuleta mapato makubwa katika halmshauri ya Kinondoni “amesema Mkuchu.

Aidha amesema ujenzi wa bustani hiyo unatarajia kuanza mwanzoni mwa mwezi Januari mwaka 2022 ambapo kwa sasa Serikali ipo katika mkakati wa kumtafuta Mkandarasi wa kuweza kufanya shughuli hiyo.