Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imebainisha kuwa, katika oparesheni zilizofanyika mwishoni mwa mwaka 2024,mamlaka hiyo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola, ilikamata Kilogramu 673.2 za dawa za kulevya aina ya methamphetamine na heroin.
Ambapo kati ya dawa hizo kilogramu 448.3 ziliwahusisha raia nane kutoka nchini Pakistani,ambazo zilikamatwa katika Bahari ya Hindi zikiwa zimefichwa ndani ya Jahazi na Kilogramu 224.9 zilikamatwa kwenye fukwe za Bahari ya Hindi jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam Januari 9, 2025, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema, mafanikio hayo yamedhihirishwa na ukamataji na udhibiti wa mianya ya uingizwaji wa dawa za kulevya nchini.
Amesema, pamoja na ukamataji wa dawa hizo DCEA bado imeendelea kujikita katika kutoa elimu juu ya madhara ya dawa za kulevya, kuimarisha huduma za matibabu ya waraibu kwa kuongeza vituo vya huduma za tiba na utengamano pamoja na kuimarisha ushirikiano na wadau wa ndani na nje ya nchi.
Pia amesema kwa mwaka huu 2025,mamlaka hiyo imejiwekea vipaumbele vitakavyo husisha kuimarisha zaidi udhibiti wa dawa za kulevya, kwa kuongeza ushirikiano wa kimataifa na matumizi ya teknolojia za kisasa, kwa kufuatilia mitandao ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya.
Kipaumbeke kingine ni kutoa elimu kwa umma, ili kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na dawa za kulevya.Pia kujiepusha na biashara,matumizi ya dawa hizo na kuendelea kuwasaidia waraibu wa dawa za kulevya kupitia programu za tiba na urekebishaji katika vituo vya tiba kwa waathirika vilivyopo nchini.
Hata hivyo, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imeendelea kutoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za uhalifu wa dawa za kulevya kwa kupiga simu bure kupitia namba 119.
More Stories
Watakaokwamisha mapato Kaliua kukiona cha moto
Dkt.Gwajima aagiza kuundwa kamati za ulinzi wa watoto
Watoto wenye uhitaji wapatiwa vifaa vya shule