November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kilio cha machinga kinavyohitaji majawabu ili kuwakomboa

Na Stella Aron,TimesMajira Online

“TUNAIOMBA Serikali itungalie kwa jicho la pili sisi machinga tunahitaji kuendelea kufanya biashara kwani familia zinatugemea na tuna mikopo ambayo hatuwezi kulipa bila ya kufanyabiashara,” hivyo ndivyo alivyoanza kusema kwa masikitiko mfanyabiashara ndogo ndogo wa Gongolamboto jijini Dar es Salaam Abubakari Ngilawe.

Anasema kuwa amekuwa akifanya biashara zake katika eneo la Gongolamboto mwisho tangu mwaka 2017 hivyo amekuwa akiwasomesha watoto wake watatu ambapo kati ya mmoja amefaulu kuanza kidato cha kwanza mwakani. “Mke wangu haoni vizuri hivyo kutokana na changamoto hiyo hawezi kufanya biashara hivyo nimelazimika kukopa sh.600,000 mwezi Septemba ili niongezee mtaji wangu na tayari fedha hizo niliziingiza kwenye mtaji hivyo sielewi fedha hizo zitarudi vipi,” anasema Ngilawe.


Kilio cha Ngilawe kinawakilisha wafanyabiashara wengi wadogo wadogo ambao awali walikuwa wakifanya biashara zao kandokando ya barabara lakini wamehamishwa kwa mpango maalumu wa Serikali wa uboreshaji miji.

Ngilawe anasema kuwa mpango huo wa Serikali haupingwi isipokuwa hakuna utaratibu maalumu wa wafanyabiashara kwenda maeneo mengine na kuendelea na biashara zao. “Mfano sisi huku Gongolamboto tangu tuondolewe barabarani hatujapangiwa maeneo mengine ili tuendelee na biashara zetu na kwa hali hiyo hivi sasa tunafanya biashara kwa kujificha ili watoto wapate kula na mambo mengine yaweze kuendelea,” anasema.

Paulina Lukas naye ni kati ya mfanyabiashara wa eneo la kituo kipya Gongolamboto anasema kuwa ana watoto wanne wanaomtegemea kwani mumewe alitangulia mbele ya haki baada ya kupata ajali mwaka juzi hivyo alipewa mtaji na ndugu zake ili afanye biashara.

“Sijui nitaishi vipi na hawa watoto kwani sina mahala kwingine ninakotegemea kupata fedha kwani hiki kibada changu kilikuwa kinanisaidia sana. Tunaiomba Serikali itufikirie sisi wajane ama wanawake kwa kututengea maeneo maalumu na si kutuacha tukiwa wakiwa hatuelewi wapi tuende,” anasema.

Naye mfanyabiashara Laurent Skonza anamuomba Rais Samia Suluhu Hassan awangalie kwa jicho la pili wafanyabiashara ndogo ndogo kwani wengi wao waliondolewa barabarani hawana pa kwenda kutoka na kutokuwepo kwa maeneo maalumu.

“Tunamuomba mama yetu Rais Samia atuangalie namna ya kutusaidia na kutupeleka sisi wafanyabiashara ndogo ndogo kwani sisi wa Gongolamboto hakuna eneo maalumu ambalo limetengewa maalumu kwa ajili yetu, familia zinatutegemea kwa kila jambo,” anasema.

Skonza anasema kuwa hivi sasa wafanyabiashara wengi wameamua kuanza kufanya biashara usiku ili waweze kupata chochote na kutunza familia zao.

“Mchana tunakimbizana na askari mgambo, watoto wetu hawajui baba ana pesa ama hana; wao wanachojua ni kupata mahitaji yao na ndio maana tumeamua kufanyabiashara usiku ili tupate chochote, hata hivyo tunaiomba Serikali itutengee maeneo ambayo sisi tutafanya biashara zetu bila ya usumbufu wowote na kwa amani kwa kipindi chote.”

“Tunafanya biashara usiku lakini bado hatuna amani kabisa, tumeamua kutengeneza meza na kila tunapomaliza biashara kila mmoja hufanya usafi na kuondoka na meza yake naamini kwa hili Serikali inaweza ikajifunza kitu,” anasema.

Naye Zaina Alfan ambaye mfanyabiashara wa matunda kwa kipindi cha miaka 7 anaiomba Serikali iwaachie wapange biashara zao kwa mtindo ambao anaamini kuwa utakuwa mzuri na hautaingia maeneo ya barabara.

“Tunaiomba Serikali kupitia kwa viongozi wetu tuendelee kufanya biashara kwa kutumia meza bila kuingia maeneo ya watembea kwa miguu ili tuweze kuwasomesha watoto wetu na sisi kulipa mikopo tuliyochukua,” anasema.

Katibu wa wafanyabiashara ndogo ndogo Gongolamboto Rajabu Issa anasema kuwa wafanyabiashara ndogo ndogo wapo njia panda hadi sasa hawaelewi ni wapi watakwenda kufanyabiashara kwani awali Gongolamboto ilitengewa eneo la Kigilagila lakini ilishindikana kwa sababu mazingira hayakuwa rafiki.

“Mara ya pili tulitakiwa kuhamia Majowe eneo la Viwege kwa Mpemba lakini nako ilishindikana na mara ya tatu tumetakiwa kuhamia eneo la Kilitex lakini cha kushangaza eneo hilo si rafiki kwa wafanyabiashara.

“Tunatakiwa tuhamie hapo lakini miundombinu yake si rafiki kwa mfanybiashara kwani hakuna choo, maji na pia eneo hilo hutumika kumwaga matope yanayotengenezwa katika daraja la Ulongoni B hivyo kipindi cha mvua ukikanyaga unadidimia.

“Tunaiomba Serikali kama imedhamiria kutusaidia sisi wafanyabiashara basi eneo hilo liboreshwe pamoja na magari ya abiria ‘daladala’ kituo cha mwisho kiwe Kilitex tunaamini kama hayo yatatekelezwa basi hata sisi tutafanya biashara zetu bila ya usumbufu na kwa amani,” anasema.

Issa anasema kuwa ofisi ya machinga Gongolamboto iliingia mkataba na Benki ya Equity ili wafanyabiashara wapate huduma ya mikopo lakini tangu kuondolewa kwako hakuna namna ya kuwapata hivyo tunaiomba Serikali itusikilize kilio chetu hata kwa kuboresha eneo lililotengwa na wafanyabiashara wakaendelea na biashara zao.

“Equity ilitoa mikopo zaidi ya milioni 10 kwa wafanyabiashara ndogo ndogo wa Gongo la Mboto kwa udhamini wa ofisi. Asilimia kubwa ya wafanyabiashara bado wanadaiwa hivyo tunaomba wakati jitihada za kuboresha maeneo hayo zikifanyika pia kuwepo kwa mtaratibu mzuri wa wafanyabiashsra kuendelea na biashara zao na si kukimbazana na askari mgambo kwani inasababisha hasara kubwa,” anasema katibu huyo.

Anasema kuwa ni vyema utaratibu wa kufanya biashara kwa meza ukafanyika kwani inakuwa ni rahisi kwa mfanyabiashara anapomaliza kuondoa meza na kisha kufanya usafi katika eneo lake kuliko kuwaacha kama watoto yatima.

“Sisi viongozi tupo tayari kuwasimamia wafanyabiashara kufanya biashara zao kwa kutumia meza na si kujenga vibanda na bila kuingia barabarani na kuendelea kulipia vitambulisho vyao vya ujasiriamali, hivyo tunaiomba Serikali isikilize maombi yetu,” anasema.

Naye mwenyekiti wa wafanyabiashara ndogo ndogo Gongolamboto wilayani Ilala mkoani Dar es Salaam Christopher Kidiga, ambaye ana miaka 20 tangu ajikite kwenye biashara ndogo ndogo anasema, “Tupo tayari sasa kujipanga kwani baada ya vibanda kuondolewa barabarani maeneo yaliyobaki ni makubwa ambayo yanaweza yakatumika kwa kupanga meza tu na wafanyabiashara wakaendelea na biashara zao.

“Tunaiomba Serikali iliangalie kwa mapana suala kwani wafanyabiashara wengi wanategemea biashara zao katika kutunza familia na hata pia ofisi yetu iliwadhamini ili kupata mikopo, tunaamini tunaweza tukasimamia suala hili na biashara kuendelea.

“Wafanyabiashara ndogo ndogo wanafuata kwenye mkusanyiko wa watu hivyo maeneo tuliyopangiwa bado mazingira si rafiki kwa wafanyabiashara na wakati hayo yakiendelea kutekelezeka tunaiomba Serikali wafanyabiashara waendelee kufanya biashara zao kwenye meza kwani kuendelea kusubiri wakati maeneo hayo yakifanyiwa ukarabati inaweza ikachukua muda mrefu na je, wafanyabiashara wataishi vipi na familia zao?” anasema mwenyekiti huyo.