Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
KAMPUNI ya huduma za kifedha kwa njia ya simu, Mixx imeendelea na dhamira yake ya kusogeza huduma zake za kifedha kwa njia ya kidigitali kupitia Kampeni yake ya ‘Kila hatua Mixx’.
Kampeni hiyo sasa imezinduliwa Kanda ya Kaskazi kwa ajili ya kuchochea ujumuishwaji wa kifedha nchini.
Safari ya Mixx ilianza rasmi mwaka 2010 ikiwa na ndoto kubwa ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata fursa ya kushiriki kikamilifu katika huduma za kifedha.
Akizungumza mara baada ya Kampeni hiyo kuzinduliwa leo, Kaimu Mkurugenzi wa Yas Kanda ya Kaskazini, Daniel Mainoya amesema baada ya Miaka 15 ndoto hiyo imekua na leo hii Mixx ni jukwaa la kifedha linalowaongoza mamilioni ya Watanzania kuelekea kwenye uchumi wa kidigitali.
Mainoya amesema, mpaka sasa Watanzania zaidi ya milioni 20 wanatumia Mixx kila mwezi kufanya miamala ya kifedha yenye thamani ya takribani shilingi trilioni 6.

Aidha, amesema kupitia mtandao wa mawakala zaidi ya 200,000, wamewezesha ajira zisizo za moja kwa moja kwa maelfu ya vijana nchi nzima.
Pia, amesema wafanyabiashara zaidi ya 500,000 wanapokea malipo salama kidigitali kupitia mifumo ya Mixx.Taasisi na makampuni zaidi ya 3,000 hutumia Mixx kwa makusanyo na malipo makubwa ya kifedha.
Hata hivyo amesema, wateja zaidi ya milioni 6 wamepata mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 1.Na kwa kuendeleza utamaduni wa akiba, wamewawezesha Watanzania kuweka zaidi ya shilingi bilioni 600.

“Kama mnavyofahamu Kanda ya Kaskazini ina upekee wa namna yake unaojulikana duniani kote kama kitovu cha utalii kutokana na vivutio vyake vya kimataifa.
*Kanda hii na hususani mkoa wa Arusha ni ngome ya kilimo cha biashara, hususan mazao ya kahawa, mbogamboga na maua yanayouzwa ndani na nje ya nchi.

“Kwa msingi huu, tunaona uzinduzi wa kampeni yetu jijini Arusha kama ishara ya dhati kwamba Mixx inataka kuhakikisha sekta muhimu kama utalii na kilimo zinakuwa na huduma thabiti na salama za kifedha,” amesema Mainoya.
Mbali na hivyo, pia amesema Kampeni hya ‘Kila Hatua Mixx’ inalenga kuchochea ujumuishwaji wa kifedha na kuunga mkono maendeleo ya uchumi wa kidigitali, hasa kwa makundi muhimu kama vijana na wanawake.
Amesema, kupitia huduma za mikopo, akiba, bima na uwekezaji, wanataka kuhakikisha kila mmoja anapata nafasi ya kushiriki katika safari ya maendeleo.
Mixx ni rafiki na mwezeshaji wa kifedha kwa kila Mtanzania, na hasa kwa wananchi wa Arusha na Kanda ya Kaskazini ambao shughuli zao za kiuchumi zinagusa dunia nzima.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi