December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kikwete aikumbuka STAMICO usiku wa Madini

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Jakaya Kikwete amelitaka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuwaendeleza wachimbaji wadogo ili waweze kukua katika uchimbaji na biashara ya madini kwa kuwashirikisha kikamilifu katika kuleta tija kwenye mnyororo wa thamani wa madini.

Hayo ameyasema alipokuwa anawahutubia washiriki wa Mkutano wa Nne wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini wakati wa Hafla ya Usiku wa Madini iliyofanyika jijini Dar es salaam .

Amelitaka Shirika hilo kuendelea kutengeneza mazingira ya kuwaimarisha na kuwasaidia wachimbaji wadogo katika mahitaji yao ili kuweza kuongeza uzalishaji katika shughuli zao za uchimbaji.

Amesema ana imani na STAMICO ya sasa, kwa kuwa ni mpya na ina utofauti na ile ya kipindi alipokuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini ambapo alitumia muda wake kuwatembelea wachimbaji wadogo ili kubainisha, kutambua na kusaidia kutatua changamoto za wachimbaji wadogo waliopo Chunya, mkoani Mbeya bila ushirikiano mahususi kutoka STAMICO.

Amesema ni wakati mzuri sasa kwa Serikali kushirikiana na wachimbaji wadogo kwa sababu, wakishirikishwa vizuri nao watakuwa tayari kushirikiana na Serikali na kuifanya Sekta Ndogo ya Uchimbaji Mdogo kuwa na tija.

Dkt. Jakaya amekumbushia jitihada za Serikali katika kubainisha changamoto za wachimbaji wadogo hususani upande wa masoko, sambamba na hatua mbalimbali zilizo tumika kurasimisha biashara ya madini ambazo zimeonesha matunda makubwa hivi karibuni na mepelekea sekta hiyo kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa.

Amefarijika sana kuona Sekta ya Madini inafanya kazi nzuri kiasi cha kuweza kushindana na Sekta ya Utalii ambayo kwa muda mrefu imekuwa ndio inaongoza kwa kuchangia Pato la Taifa.

Naye, Waziri wa Madini Mhe. Dkt. Doto Biteko ametumia fursa hiyo kuwashukuru Mawaziri wote waliotangulia kuhudumu katika Wizara hiyo na kusema jitihada na michango waliyoitoa katika kuendeleza Sekta ya Madini ndio imeifanya Wizara hiyo kufanya vizuri na kuwa miongoni mwa sekta zinazofanya vizuri katika kuchangia Pato la Taifa.

Amewataka wachimbaji wakubwa na wadogo kuzingatia yale yote ambayo yamejadiliwa katika mkutano huo ili kuweza kuleta tija katika shughuli zao za uchimbaji madini, kuimarisha Sekta ya Madini sambamba na utunzaji Mazingira.

Kwa upande wa STAMICO, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala Bw. Deusdedith Magala, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO amesema yale yote yaliyozungumwa yamechukuliwa kama chachu na hamasa katika kuboresha majukumu yake kwa ya wachimbaji wadogo.

Jitihada zilizoanzishwa tangu miaka ya zamani ndio imefungua milango ya kuliwezesha Shirika kupenya na kuwafikia wachimbaji wadogo kwa urahisi na kuleta umoja na ushirikiano uliopo kwa sasa.