Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mongolandege, Rajabu Tego amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufungua milango kwa kutoa miongozo yenye unafuu katika usajili wa vikundi mbalimbali kisheria.
Hayo ameyasema leo Juni 16, 2024 jijini Dar es Salaam wakati wa kukabidhi katiba, kanuni na kadi ya mwanachama wa kikundi cha Tunaweza ambapo alikuwa mgeni rasmi.
“Ni jambo la kumpongeza Rais Samia kuanzisha miongozo hiyo kwa vikundi vya kijamii, lakini nakipongeza kikundi cha Tunaweza ambacho kimepata usajili hivyo hata michango wanayotoa itakuwa mahala salama na kuwezesha kikundi kupata maendeleo na hata kwa mwanachama mmoja mmoja pindi inapotolewa mikopo” amesema.
Naye Katibu wa kikundi hicho cha Tunaweza, Gervas Paulo, amesema kuwa kikundi hicho kina wanachama 118 ambapo kilianzishwa Machi 8, 2023.
“Kikundi cha Tunaweza tayari kimepata usajili, na leo tumegawa katiba kwa wanachama ili kila mmoja afahamu sheria na kanuni tulizojiwekea ili kuepuka kwenda kinyume na taratibu za makubaliano yetu” amesema.
Katibu huyo amesema kuwa kikundi hiki kimeanzishwa kwa nia ya kusaidiana katika nyanja mbalimbali lakini pia katika kutoa misaada kwa watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu.
“Tunashirikiana katika makundi hayo na wanachama wamekuwa wakichangia ada ya sh.5,000 kwa kila mwezi na kuhifadhiwa benki ingawa bado kuna baadhi ya wanachama wako nyuma katika uchangiaji jambo ambalo wanakwenda kinyume na katiba yetu,” amesema.
Ameongeza kuwa kuna mafanikio mbalimbali ambayo yamepatikana lakini pia kuna changamoto ya kuwepo kwa baadhi ya wanachama ambao si waaminifu wenye mtazamo hasi wa kuomba kupata matatizo ili wapate fedha tu hivyo tunashauri ni vyema wote tukawa wazalendo.
Naye katibu msaidizi Ramadhan Mtuli, amesema kuwa kikundi cha Tunaweza kinapokea wanachama kutoka maeneo mbalimbali ili mradi mwanachama awe na akili timamu.
“Tunapokea wanachama kutoka maeneo mbalimbali ili mradi awe na akili timamu hivyo tunawakaribisha wenye nia ya kutaka kujiunga na Tunaweza kwani ni kikundi kilichosajiliwa kisheria,” amesema.
Hata hivyo amempongeza Rais Samia kwa kazi nzuri na kubwa anazozifanya hivyo rai yao kwake ni kuomba kuwafikia katika utaratibu wa utoaji mikopo ili wanachama waweze kunufaika na kupata maendeleo.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba