May 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kikundi cha Mwanamke Shujaa chamchangia Fedha ya kuchukua Fomu Rais Samia

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Rungwe

KIKUNDI cha mwanamke Shujaa kilichopo wilayani Rungwe Mkoani Mbeya  kimekabidhi zaidi  ya shilingi milioni 1 Mkuu  wa wilaya hiyo, Jaffar Haniu ili ziweze kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan wakati wa zoezi la uchukuaji wa fomu ya kugombea Urais mwezi Oktoba mwaka huu .

Akipokea fedha hizo Mei 6,2025, Mkuu wa wilaya ya Rungwe, Jaffar Haniu amekishukuru kikundi hicho kwa moyo wa uzalendo waliouonesha na kwa kufanya hivyo imedhirisha wananchi walivyo na mshikamano na mapenzi mema kwa Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania Dkt
.Samia Suluhu Hasasan.

“Kitendo hichi kinadhihirisha ni jinsi gani wananchi wa wilaya hii ya Rungwe walivyo na imani na Rais Samia ,huu ni uzalendo wa hali ya juu Sana kwa wananchi wetu”amesema Mkuu huyo wa Wilaya.

Naye Mwenyekiti wa Kikundi cha Mwanamke Shujaa ,Greda  Mwakabumbe amesema kuwa wazo la kumchangia Rais liliasisiwa siku ya Mwanamke Duniani ambapo wanakikundi walianza kuchanga kidogokidogo mpaka kufikisha kiwango hicho cha fedha.

Mwakabumbe ameongeza kikundi hicho kimefikia hatua hiyo baada ya kuridhika na namna Rais alivyoibadilisha miundombinu ya elimu, afya, kilimo na usafirishaji hatua iliyokuza uchumi wa wananchi pamoja na ustawi wa jamii.

“Aliyofanya Mama yetu ni  mambo makubwa hivyo tuna kila Sababu ya kumsapoti kumchangia fedha hii ili wakati ukifika wa kuchukua zimsaidie,kwa wilaya yetu hii ya Rungwe amefanya mambo mengi “amesema Mwenyekiti huyo.

Kikundi hicho  chenye wanachama 27 pamoja na ujasiriamali pia hujishughulisha na umoja wa kuweka Akiba na Kukopeshana fedha.