March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kihongosi:CCM haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya kiongozi mzembe

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

KATIBU  wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenan Kihongosi, amesema Chama Cha Mapinduzi(CCM) hakitasita kuchukua hatua kali dhidi ya kiongozi yeyote atakayeshindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Kihongosi amesema hayo jijini hapa leo Novemba 19,2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mustakabali wa Chama hicho baada ya kukamilika kwa uchaguzi na kuunda dola huku kikisema kutakuwa na mageuzi makubwa na kuwakumbusha Mawaziri na Manaibu waziri walioapishwa jana kuwa kinatarajia utendaji wa juu na matokeo yanayoonekana kuwa  uteuzi wa viongozi hao ni dhamana kubwa waliyopewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, hivyo hawapaswi kuichukulia kwa urahisi.

“Chama kinawataka mawaziri na manaibu waziri waende kufanya kazi kwa weledi na wasiende kumuangusha Rais. Wengi ni wapya, hivyo pamoja na kufurahia uteuzi, wakumbuke kuwa Rais hana mchezo. Anataka kazi, matokeo na utendaji uliotukuka unaozingatia utu kwa Watanzania wote,” amesema  Kihongosi.

Kihongosi alisisitiza kuwa Chama hicho kinakwenda kusimamia serikali na si serikali kukusimamia Chama na hakitakuwa na msalie mtume na viongozi wazembe, wavivu na wala rushwa.

“Chama cha Mapinduzi hakitasita kuchukua hatua kali kwa kiongozi yeyote mzembe ndani ya Serikali. Tunataka wote walioteuliwa waende wakawatumikie wananchi na si vinginevyo,” amesisitiza

Pamoja na hayo Kihongosi amewasihi watanzania kulinda amani kwa kuwapuuza na kuwakataa watu wasioitakiwa mema nchi na wanaohamasisha uvunjifu wa amani.