Na Isaack Zenda,Timesmajira
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi amesema chama hicho kimeleta wagombea waliobeba matarajio na nia thabiti ya kutatua changamoto za watanzania.
Pia amesema chama kimeleta wagombea bora na wenye uzoefu wa kutosha ndani ya Chama na Serikali.
Kihongosi alieleza hayo leo Agosti 27,2025 wakati akizungumza na vyombo vya habari katika viwanja vya Tanganyika Packers Kawe Wilaya ya Kinondoni Dar es salaam kuhusu uzinduzi wa kampeni za chama hicho unaotarajiwa kufanyika hapo kesho.
“Ukichukua wasifu wa Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi, Dkt Samia Suluhu Hassan utaona wasifu umesheheni mambo mengi makubwa pia ukichukua wasifu wa mgombea mwenza Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi wasifu umesheheni uzoefu wa kutosha,” amesema Kihongozi.
Kihongosi, amewakaribisha wananchi wa Dar es Salaam kushiriki kwenye uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mkuu, ambapo mgombea urais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na mgombea mwenza wake, Dkt. Emmanuel Nchimbi, watazindua rasmi safari ya kuelekea ushindi wa chama hicho.
Amesema kuwa hafla hiyo ni mwanzo wa kampeni ambazo zitajikita katika kueleza mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya CCM 2020–2025 pamoja na kuibua dira mpya yenye majibu ya changamoto zinazowakabili Watanzania katika sekta mbalimbali.
“Kwa mwaka 2025–2030, Chama Cha Mapinduzi kimekuja na Ilani kubwa iliyobeba matumaini ya Watanzania. Ilani hii siyo tu dira, bali ni nyenzo ya kweli ya kutatua changamoto zinazomgusa kila mwananchi wa kawaida,”amesema.
Aidha, Kihongosi ameipongeza CCM kwa kutoa wagombea wenye uzoefu mkubwa wa kiuongozi na kisiasa, akisisitiza kuwa wasifu wa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Dkt. Emmanuel Nchimbi unadhihirisha ukomavu, weledi na ubobezi wa kisiasa.
“Ukichunguza wasifu wa mgombea urais wetu, Dkt. Samia, utabaini ni kiongozi mwenye rekodi ya mafanikio makubwa katika serikali na chama. Vilevile, Dkt. Nchimbi ni kiongozi mwenye uzoefu wa kutosha kushirikiana naye kuongoza taifa. Hii ni ishara kuwa CCM imewaletea Watanzania wagombea bora kabisa,”amesisitiza.
Kihongosi amesema kuwa kampeni za CCM mwaka huu zitafanyika kwa misingi ya kistaarabu, zikijikita kwenye hoja na sera bila kejeli au kudhalilisha utu wa mtu mwingine. “Tunatambua kuwa Tanzania ni nchi ya amani, umoja na mshikamano. Hivyo, kampeni zetu zitaheshimu utu wa kila mmoja na kulinda maslahi ya taifa,”amesema.
Aidha, CCM itawanadi wagombea ubunge kwa majimbo 12 ya Dar es Salaam pamoja na wagombea wa nafasi za udiwani, ambapo viongozi mbalimbali wa chama, viongozi wa dini, wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) pamoja na wadau wengine muhimu wanatarajiwa kushiriki kwenye uzinduzi huo.
Akihitimisha, Kihongosi amesema: “CCM itaendelea kusimama kidete kulinda Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuheshimu vyombo vya ulinzi na usalama na kuhakikisha kampeni hizi zinabaki kuwa za kistaarabu na zenye tafsiri halisi ya mshikamano wa kitaifa.”

More Stories
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI