January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kigoma Ujiji yampongeza Samia kwa mradi wa maji

Na Allan Vicent, Timesmajiraonline,Kigoma

MAMLAKA ya Maji na Usafi wa Mazingira Kigoma (KUWASA) imempongeza Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia zaidi ya sh. bil 40 kwa ajili ya kutekeleza mradi mkubwa wa chanzo cha maji chenye uwezo wa kuzalisha lita mil 42 kwa siku.

Chanzo hicho cha ziwa Tanganyika kilichopo eneo la Amani Beach katika kata ya Bangwe Mjini Kigoma kimekamilika kwa asilimia 100 na maji yameanza kusambazwa kwa wakazi wa kata zote 19 zilizopo katika manispaa hiyo.

Akiongea na mwandishi wetu kwa niaba ya Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo Poasi Kilangi, Mkuu wa Idara ya Utumishi Paskazia Nyalaja, alisema kuwa kukamilika kwa mradi huo kumeleta faraja kubwa kwa wakazi wa manispaa hiyo.

Alibainisha kuwa mradi huo ambao umegharimu zaidi ya sh bil 40 ni mkombozi kwa wananchi kwa kuwa utakidhi mahitaji yote ya maji kwa wakazi wa manispaa hiyo, kazi iliyoko mbele yao sasa ni kusambaza huduma hiyo katika kata zote.

“Tunamshukuru sana mama yetu, Rais Samia kwa kutupatia fedha za kutosha kwa ajili ya mradi huo na kuendelea kutuletea fedha zaidi ili kuhakikisha kata zote 19 zinafikishiwa huduma ya maji safi na salama,” alisema.

Naye Mkurugenzi wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira wa Mamlaka hiyo Sigfried Shaushi alimshukuru sana Rais kwa kumaliza kero ya maji katika Mji huo na kuwahakikishia wananchi kuwa kero yao sasa itabakia historia.

Aidha, alimshukuru Rais kwa kuwapatia zaidi ya sh. bil 1.7 kwa ajili ya kupanua mradi huo ili kufikisha huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa Mtaa wa Kamara katika kata ya Bangwe, mradi ambao utanufaisha wakazi zaidi ya 75,000.

Mhandisi Shaushi aliongeza kuwa kukamilika kwa chanzo hicho kikubwa cha maji kumewezesha upatikanaji huduma ya maji safi na salama katika Manispaa hiyo kuongezeka kutoka asilimia 80 hadi 92 katika kipindi cha miaka 3 ya Rais Samia.

Alibainisha kuwa kwa mwaka ujao wa fedha Mamlaka hiyo imetenga kiasi kingine cha sh bil 11 kwa ajili ya kufikisha huduma hiyo katika kata 4 zilizopo pembezo mwa Manispaa hiyo ambazo ni Simbo, Mngonya, Ziwani na Kagunga.

“Tunamshukuru sana Rais kwa kuendelea kutuletea fedha za kutosha ili kuhakikisha miradi yote inatekelezwa kwa ufanisi mkubwa na kwa kiwango kinachotakiwa na kuikamilisha kwa wakati’, alisema.

James Mhange mkazi wa Mtaa wa Kamara, Kata ya Bangwe katika Manispaa hiyo alisema kuwa kukamilika kwa mradi huo kumeleta shangwe na furaha kwa wananchi kwa kuwa sasa wanapata huduma ya maji safi ya bomba wakati wote.

Alieleza kuwa awali afya zao zilikuwa hatarini kwa sababu walikuwa wanakunywa maji ya ziwani ambayo sio safi na salama na walikuwa wanapata magonjwa ya kuharisha mara kwa mara jambo lililokuwa likiibua malalamiko mengi.

Wakazi wa Mji Mwema katika Manispaa hiyo, Rehema Nelson na Festo Francis walimshukuru sana Rais Samia kwa kusikia kilio chao na kupeleka kiasi hicho cha fedha ili kutekelezwa mradi huo mkubwa wa chanzo cha maji.