March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kigalu azikwa nyumbani kwake Kijiji cha Itilo

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online -Tabora

ALIYEKUWA Diwani wa Kata ya Itilo na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Nzega mkoani Tabora, Paschal Kigalu (56),amezikwa nyumbani kwake Kijiji cha Itilo wilayani Nzega aliyefariki kwa ajali ya gari iliyotokea juzi wilayani humo.

Akitoa salamu za chama kwenye ibada ya mazishi iliyofanyika jana nyumbani kwa marehemu, Kijiji cha Itilo, Kata ya Itilo, Wilayani Nzega, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Mkoa wa Tabora Saidi Nkumba, amesema Diwani huyo alikuwa mstari wa mbele kutetea maslahi ya wana Itilo na kusimamia maendeleo ya halmashauri hiyo.

“Hili ni pigo kwa Chama Cha Mapinduzi na serikali, tumepoteza mtu muhimu katika kipindi ambacho wananchi ndo walikuwa wameanza kuonja ahadi alizotoa kwenye kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29 mwaka jana,”amesema Nkumba.

Nkumba amewataka wanaCCM na wakazi wa Kata hiyo kuwa watulivu katika kipindi hiki cha majonzi, huku akiwahakikisha kuwa wakati ukifika taratibu zitafanyika ili kumpata mrithi sahihi atakayesimamia maendeleo ya Kata yao.

Awali akitoa salamu za Serikali, Mkuu wa Mkoa huo,Paul Chacha, ameeleza kuwa marehemu alikuwa nguzo muhimu kwa maendeleo ya halmashauri hiyo na alifanya kazi kwa ushirikiano na uelewano na watumishi wote.

Amewaomba ndugu wa marehemu kukaa vizuri na familia hiyo na kuhakikisha mjane na watoto wanapata haki zao, aidha amedokeza kuwa serikali ya Mkoa itaendelea kuwa karibu na familia hiyo hivyo kama kutakuwa na tatizo lolote wasisitize kutoa taarifa.

Akiongea kwa niaba ya familia, Mbunge wa Nzega Mjini,Hussein Bashe,ameeleza kuwa marehemu alikuwa mtu wake wa karibu, hivyo atahakikisha yale yote aliyokuwa anayasimamia yanatekelezwa kwa vitendo ikiwemo mradi wa ujenzi wa maghala ya taifa ya chakula yanayojengwa Kikanda katika Kata hiyo.

Bashe amedokeza kuwa marehemu amewahi kuwa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji,Diwani wa Kata hiyo kwa awamu tatu mfululizo, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri na Mwenyekiti wa Halmashauri hadi umauti ulimpomfika.