Na Mwandishi Wetu,Timesmajira online,Mbeya
NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara Exaud Kigahe amefanya ziara ya kutembelea maonyesho ya Kilimo na Mifugo ambayo Kitaifa yanafanyika jijini Mbeya ambapo amepata fursa ya kutembelea taasisi mbalimbali zilizo chini ya Wizara yake .
Akiwa katika banda hilo kwenye viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya Naibu Waziri huyo ameonyesha kufurahishwa na tafiti zilizofanywa na TIRDO hasa mashine ya kuchakata mafuta yanayotokana na matunda ya Parachichi na kutoa agizo kwa Uongozi wa Shirika hilo kuhakikisha wanawafikia wananchi ili tafiti zilizofanyika ziweze kuwa na manufaa kwa taifa kwa ujumla.
“TIRDO nyie ni watafiti, hapa kwenu naomba niagize kuwa mpaka Maonesho yanayofuata 2024 mje na idadi kamili ya Mikoa/Wilaya na Wadau waliofikiwa na teknolojia hii” amesisitiza Mhe.Kigahe.
Mhe.Kigahe ameeleza kuwa zao la Parachichi linalimwa katika mikoa Mingi ya nyanda za Juu Kusini na mpaka sasa matunda haya yanatumika kwa matumizi ya chakula kama matunda tu jambo ambalo limesababisha wakati mwingine soko kuwa chini na kusababisha wananchi kupata hasara.
“Nimefurahi pia kuona mmebuni mashine isiyotumia umeme ambyo ni rafiki katika mazingira yote, naomba muwafikie wananchi” aliongeza Mhe.Kigahe.
Akitoa Maelezo juu ya ufanyaji kazi wa mashine hiyo mtaalam na mtafiti kutoka TIRDO Bwana Paul Josephat Kimath amesema kuwa mashine hiyo inaweza kutumika katika mazingira yoyote bila kuhitaji nishati yoyote na amemueleza Mhe.Naibu Waziri kuwa soko la mafuta ya parachichi kwa sasa ni kubwa na hivyo anawakaribisha wawekezaji wakubwa na wadogo kuwekeza katika kuchakata mafuta haya.
Mhandisi Kimathi ameeleza kuwa mashine hiyo ina uwezo wa kuchakata hadi kilo 120 za parachichi kavu kwa siku ambapo kwa utafiti uliofanywa na TIRDO kilo tatu hadi kilo nne(kilo 3-4) ya Parachichi kavu inaweza kuzalisha lita moja ya mafuta na hivyo mashine kuwa na uwezo wa kuzalisha lita 30-40 kwa siku.
Kuhusu soko la mafuta ya Parachichi, Bwana Kimath amemueleza Mhe.Waziri kuwa soko ni kubwa na kwa sasa lita moja ya mafuta hayo yanauzwa kati ya shilingi elfu ishirini na thelathini na tano(20,000-35,000).
Mafuta ya Parachichi yanatumika kama mafuta ya kula lakini pia malighafi muhimu kwa viwanda vinavyozalisha vipodozi na dawa mbali mbali.
Shirika la utafiti na Maendeleo ya viwanda Tanzania ilianzishwa mwaka 1979 likiwa na malengo ya kufanya utafiti wa teknolojia mbali mbali, kutoa ushauri wa kitaalam serikalini , kuanzisha na kutunza taarifa za kitaalam, kusambaza tafiti pamoja na kuanzisha mifumo ya kudhibiti uchafuzi wa mazingira wakati wa uzalishaji viwandani.
More Stories
Waziri Mavunde:Benki Kuu yanunua tani 2.6 za Dhahabu nchini
Kampeni msaada wa kisheria ya mama Samia kutatua kero za kisheria Katavi
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25