January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kigahe aeleza Mkumbi utakavyokuza Biashara na Uwekezaji Nchini

Na Joyce Kasiki,Timesmamajira online,Mbeya

NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara Exaud Kigahe amesema,tangu kuanzishwa kwa Mpango wa Kuboresha Mazingiraya Biashara na Uwekezaji (MKUMBI)  2019, na maboresho mbalimbali yameendelea kufanyika ikiwa ni Pamoja na kupitia sheria na kutunga sheria nyingine pamoja na kanuni zake ili ziweze kuvutia zaidi wawekezaji na ufanyaji biashara hapa nchini.

Akizungumza jijini Mbeya alipofanya ziara kwenye maonyesho ya Kitaifa ya Wakulima Nane Nane ,Kigahe amesema,moja ya sheria hizo ni pamoja na sheria ya Uwekezaji na mwaka 2022.

“Kwa hiyo tangu kuanzishwa kwa mpango huu tumendelea kufanya maboresho mbalimbali na moja ya sheria zilizopitishwa na bunge na kusainiwa na Rais Samia Suluhu Hassan ni Pamoja na sheria ya uwekezaji ya  mwaka 2022 ambayo pamoja na mambo mengine imeweka maboresho ya kuweka vivutio maalum kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi kwa kupunguza mitaji inayohitajika ili wapate vivutio hivyo.”amesema Kigahe na kuongeza kuwa

“ Lakini zaidi tumeweza kuunganisha mamlaka ambazo zilikuwa zinaingiliana kama Mamlaka ya Udhibiti wa Chakula na Vipodozi  (TMDA ) na Wakala wa Viwango Tanzania (TBS)  na kuboresha ili kupunguza muingiliano wa majukumu katika mamlaka hizo.”amesema Kigahe na kuongeza kuwa

“Lakini tozo na kodi nyingi zimefutwa ambazo zilikuwa zinaleta ukinzani katika kuboresha biashara , kodi hizo zimefutwa katika sekta ya kilimo ikiwemo tozo mbalimbali zilizokuwa zinahusika na mazao ya biashara na kilimo ambayo mkulima alikuwa analazimika kulipa tozo hizo.”

Naibu Waziri huyo amesema,maeneo mengi katika sekta ya kilimo na misitu kodi yake ilikuwa asilimia tano huku akisema  sasa imepungua hadi asilimia tatu .

“Hii imeongeza watu kufuata sheria na kanuni zilizopo kwa uhiari bila kulazimishwa, kwa hiyo wanalipa kodi kwa hiari kwa sababu imekuwa ni rafiki na inayoendana na uhalisia,lakini pia sasa tunajenga mfumo ambao unaunganisha taasisi zote zinazohusika katika kusajili biashara ambao ni wa kidigitali.”

Kwa mujibu wa Kigahe mfumo huo unahusisha zaidi ya taasisi mbalimbali  kikiwemo kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC) ,Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA),Mamlaka ya Mapato Tanzaia(TRA),Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Uhamiaji.

“Kwa hiyo mtu akiingia kwenye dirisha moja hilo maana yake atapata hivyo vibali vyote kwa mara moja,lakini lengo ni kuhakikisha hapo baadaye tunaunganisha taasisi zote ili mtu akitaka kupata kibali hata cha Baraza la Mazingira (NEMC) aingie hapo badala ya kutoka kwenye taasisi moja na kwenda kwenye taasisi nyingine.”amesema Naibu Waziri huyo na kuongeza kuwa

“Kwa hiyo nadhani hii ni moja ya maboresho ambayo serikali imeendelea kuyafanya ili kuboresha biashara kupitia MKUMBI ambapo Serikali ya awamu ya sita imesema na hili ndiyo lengo kuona kwamba sekta binafsi inakuwa ndiyo sekta kiongozi katika kuendesha uchumi na kufikia lengo la kufikia uchumi wa kati wa juu kupitia viwanda.”

Aidha amesema,maboresho yanayofanyika kupitia MKUMBI  yataenda kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi lakini pia kuvutia wawekezaji zaidi kutoka sekta binafsi ndani na nje ya nchi katika sekta zote  ikiwemo viwanda,biashara,utalii, madini, kilimo, uvuvi na sasa tuna uchumi wa Buluu.

Amesema,Serikali inaamini mazingira ya ufanyaji biashara yakiboreshwa na sekta binafsi ikakua ,itachangia katika kuongeza ajira kwa vijana na watanzania kwa ujumla wake lakini pia itaongeza mapato ya nchi hasa fedha za kigeni ambazo zinahitajika sana katika kuingiza bidhaa ambazo Tanzania hatuzalishi.

Aidha Kigahe amesema hatua hiyo pia itaongeza uwekezaji katika viwanda ili kuchakata na kuongeza thamani mazao ya kilimo ambayo sekta ya kilimo inaajiri watanzania wengi na hivyo kuleta tija kwenye mazao wanayoyazalisha.

Amewataka wadau kutoka serikalini na sekta binafsi waendelee kutoa maoni kuhusiana na kuendelea kutekeleza mpango huo wa kuboresha ufanyaji biashara hapa nchini maana huenda changamoto zikaibuka wakati wa utekelezaji wa mpango huo ambao unapaswa kuwa endelevu.

“Tunajua kadri tunavyotekeleza kuna changamoto zitaibuka na mpango huu lazima uwe endelevu na lengo la serikali ni kuona tunatatua changamoto zote ambazo zinaikumba sekta binafsi katika kufanya biashara hapa nchini na hatimaye tufikie lengo la kuwa na uchumi wa kati wa juu ambalo ndilo lengo la Rais Samia ili watanzania wengi waweze kunufaika na uchumi wa nchi hii.”amesisitiza Kigahe