*Polisi waendelea na uchunguzi
*Mtuhumiwa ajitambulisha kuwa mke wa mjomba wa mama mzazi
Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
Mtoto wa siku moja wa jinsia ya kike anadaiwa kuibwa na mtu ambaye alijitambulisha kuwa ni mke wa mjomba wa mama mzazi wa mtoto huyo,Kata ya Buzuruga wilayani Ilemela mkoani Mwanza.
Huku Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linaendelea kufanya uchunguzi  ili kubaini chanzo cha tukio hilo na kumkamata mwanamke huyo anayedaiwa kumuiba mtoto huyo.
Akizungumzia tukio hilo Februari 9,2026,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbord Mutafungwa,amesema tukio la wizi wa mtoto mchanga mwenye umri wa siku moja lililotokea Februari 7,2026 majira ya saa 10 jioni (16:00hrs) huko Buzuruga, wilaya ya Ilemela jijini Mwanza.
Mutafungwa amedai kuwa Februari 6,2026 majira ya saa 12 jioni (18:00hrs) mwanamke aitwaye Nice Ajuna Renatus(24), mkazi wa mtaa wa Nyasaka Msumbiji, alifika katika kituo cha afya Buzuruga kujifungua.
 Amesema,mwanamke huyo alijifungua salama mtoto wa jinsia ya kike na kupewa mapumziko katika chumba namba 4 kwenye kituo hicho cha afya.Â
Akiwa amepumzika ndipo alifika mwanamke jina halijafahamika umri wake unakadiriwa kuwa kati ya miaka 35 au 40 nakujitambulisha kuwa ni mke wa mjomba wake na alifika kwa ajili ya kumuona.Mwanamke huyo alitoa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na kumpatia chai.
Hivyo ilipofika Februari 7,2026 majira ya saa 11 jioni(17:00hrs),Nice(mama wa mtoto),akiwa na kichanga chake cha siku moja aliruhusiwa kutoka hospitali baada ya hali yake ya kiafya kuwa sawa.
Hata hivyo wakati anaondoka hospitalini hapo kuelekea nyumbani ndipo mwanamke aliyejitambulisha kuwa ni mke wa mjomba wake alimuomba amsaidie kubeba mtoto ili waelekee nyumbani,wakiwa njiani alimpitisha vichochoroni hadi kwenye nyumba ambayo alidai kuwa ni nyumba yake.
“Alizunguka nyumba akidai anatafuta funguo ili waingie ndani kisha akatoweka na mtoto kusikojulikana. Mama mzazi wa mtoto alibaki nje ya nyumba hiyo hadi alipoanza kutiliwa wasiwasi na familia ambao ni wamiliki halali wa nyumba hiyo, ndipo ikabainika kuwa, mama huyo alikuwa ameibiwa mtoto wake mwenye umri wa siku moja na taarifa kufikishwa kituo cha polisi,”amesema Mutafungwa.
Sanjari hayo Mutafungwa,ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza hususani akina mama kuchukua tahadhari na kuacha tabia za kuamini watu wasiowafahamu na kuwakabidhi watoto ili wawashikie badala yake wasaidiwe na watu, ndugu, jamaa na marafiki wanaowafahamu.
“Jeshi la polisi tunatoa witi kwa yeyote mwenye taarifa zinazoweza kusaidia kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo na kupatikana kwa mtoto asisite kuziwasilisha kituo chochote cha polisi,”amesema Mutafungwa.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina