Sophia Fundi,Timesmajira Online, Karatu
Simanzi, vilio vyatawala ndani ya kanisa la Mtakatifu Bikira Maria wa mitume, Parokia ya Karatu Jimbo katoliki la Mbulu, kufuatia mauaji ya Paroko wa Parokia hiyo Padri Pamphili Nada tukio lililotokea majira ya saa 9 usiku wa kuamkia leo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Askofu wa Jimbo hilo, Anton Lagwen wakati wa adimisho la Misa takatifu alisema, marehemu aliuawa kwa kupigwa na mtu anayedaiwa kuwa na upungufu wa akili ambaye alifika kanisani hapo usiku wa saa tisa huku akimuomba mlinzi Paulo Qamara kumfunguliwa mlango wakwa ajili ya kusali.
Taarifa hiyo, pia ilieleza kuwa baada ya usumbufu wa muda mrefu, marehemu alikwenda kwa mlinzi na kumsihi aongee naye kwa upole kwani anaonekana kuwa na upungufu wa akili.
Hata hivyo, marehemu alikubali kumfugulia mlango mtu huyo anayedaiwa kuwa na upungufu wa akili kuingia ndani ya kanisa na kumkuta Paroko ndani ya Kanisa.
Katika Hali isiyo ya kawaida kichaa huyo alifunga mlango kwa ndani na kumfungia mlinzi nje na kubaki na marehemu ambapo alimpiga na chuma kichwani na kumwua.
Baada ya mlinzi kuona Hali hiyo alipiga kengele ya kuita waumini walioko jirani na kanisa kwa msaada ambapo walifanikiwa kumkamata, kumpiga na kumwua.
Aliyeuawa ambaye anadaiwa kuwa ni mwenye upungufu wa akili amejulikana kwa jina la Romani Leonard ( 30), mkazi wa Gyekrum Lambo wilayani hapo.
Askofu Lagwen aliwaomba waumini kuachia kitendo hicho kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya na kuendelea kumwombea marehemu Padre Pamphili kwani amemaliza safari yake ndani ya Kanisa alilokabidhiwa.
“Tuwe wavumilivu katika kipindi hichi, tuendele kumwombea babayetu aliyetwaliwa leo akiwa katika eneo lake la kazi, ameuawa ndani ya Kanisa, damu yake imemwagika ndani ya Kanisa, tumwombee,”amesema Askofu Lagwen.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Karatu, Dadi Kolimba amesema amepokea tukio Hilo kwa mshtuko mkubwa na aliwaomba wananchi kushirikiana na jeshi la Polisi kuandaa ulinzi shirikishi katika maeneo yao.
Kwa upande wake, Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha Justine Masejo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.
More Stories
The Desk & Chair yashusha neema Gereza la Butimba
TVLA,yapongezwa kwa kuzalisha chanjo
TAKUKURU,yasaidia kurejesha hekali 8