Na Heri Shaaban, Timesmajira Online,Temeke
Shule ya sekondari Kibasila iliyopo wilayani Temeke,jijini Dar-es-Salaam, inajivunia mafanikio ya kitaaluma kwa kufanikisha ufaulu wa asilimia 100 kwa miaka mitatu mfululizo, kutokana na kuimarika kwa kiwango cha elimu.
Akizungumza katika mahafali ya kidato cha sita, Mkuu wa shule hiyo, Mwalimu Juma Orenda,amesema mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano wa karibu kati ya walimu, wanafunzi, wazazi na uongozi wa shule.
Amesisitiza kuwa shule hiyo ina walimu mahiri, wenye uzoefu na moyo wa kufundisha, hali inayowezesha matokeo bora kwenye mitihani ya Wilaya, Kanda na Taifa.
“Tunaona fahari kila mwaka ufaulu unazidi kuimarika. Mwaka 2023, ufaulu wa kidato cha pili ulikuwa asilimia 100, kidato cha nne asilimia 98, na kidato cha sita asilimia 98. Mwaka 2024, kidato cha pili na cha nne walifaulu kwa asilimia 100, huku kidato cha sita wakifikisha asilimia 98. Haya ni matokeo ya juhudi za pamoja,”amesema Orenda.
Ameongeza kuwa shule hiyo imepunguza daraja la nne na kuondoa ziro kwa kiwango kikubwa katika mitihani ya kitaifa, huku akieleza kuwa wanamuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake katika kuboresha sekta ya elimu nchini.
Shule ya Sekondari Kibasila ni miongoni mwa shule kongwe nchini, iliyoanzishwa mwaka 1951 chini ya usimamizi wa Jumuiya ya Magoa, kwa jina la St. Francis Xvaler Chang’ombe. Ilisajiliwa rasmi kuwa shule ya serikali mwaka 1970. Kwa sasa, ina mikondo 36 kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita, ikiwa na wanafunzi 1,990 (wasichana 957 na wavulana 1,033), na walimu 65.
Katika mahafali hayo, wahitimu 265 wa kidato cha sita (wasichana 134 na wavulana 131) walikabidhiwa vyeti vyao. Mwalimu Orenda aliwataka wawe mabalozi wazuri wa shule hiyo na kuitangaza kwa mazuri yake.
More Stories
Dkt.Jingu ahimiza matumizi ya TEHAMA katika malezi
Bil.64.5 zimetengwa kwajili ya kupanga,kupima na kumilikisha ardhi halmashauri 131 nchini
LATCU Katavi yasaidia mahitaji ya Mil.5.7 kituo cha watoto yatima,mahabusu