December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kibao azikwa, maelekezo ya Rais Samia yaanza kufanyiwa kazi

Na Jackline Martin,Timesmajiraonline,Tanga

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya nchi, Mhandisi Hamad Massaun, amesema maelekezo ya Rais Dkt. Samia yameshaanza kutekelezwa na hatua zitachukuliwa Kwa wale watakaobainika kuhusika na tukio la mauaji ya aliyekuwa kada wa Chama cha Demokrasi na Maendeleo (CHADEMA) na Mjumbe wa Sekretarieti ya Taifa,Mohamed Ali Kibao

Masauni alitoa kauli hiyo jana wakati akiwasilisha salamu za Serikali katika mzishi Kibao yaliyofanyika nyumbani kwake mkoani Tanga. “Nimekuja hapa kuwapa salamu za Serikali kupitia viongozi Wakuu akiwemo Rais Dkt. Samia ambaye ameonesha kuguswa na tukio hilo, na maelekezo aliyoyatoa ili kuweza kufanywa uchunguzi Kwa haraka hatimaye wahusika Wote waweze kuchukuliwa hatuna kwa mujibu wa Sheria,” alisema na kuongeza;

“RAIS amesononeshwa, amesikitishwa na ameumizwa sana na tukio hili pamoja na Serikali nzima ni Jambo ambalo halikupaswa kutokea hasa katika nchi yetu ambayo kwa miaka yote tumekuwa tukijivunia juu ya usalama na amani ya nchi hii na mfano bora ukilinganisha na nchi zingine zinazotuzunguka Duniani,” alisema Masauni.

Aidha Waziri Masauni alitoa wito kwa Wananchi wote kuacha kushtumu na kama wana kielelezo chochote na cha mtu yoyote kuhusika na jambo hilo awasilishe Polisi ili kisaidie katika hatua zaidi za kupata wahusika na kuweza kuchukuliwa hatua.

“Serikali haijawahi na haitawahi kuvumilia jambo lolote linalokiuka misingi ya haki ya mtu ya kuishi na kufanya analotaka kufanya kwa mujibu wa Katiba inavyoonesha kwani Rais Dkt. Samia amekuwa akilisimamia hilo tangu anaingia madarakani,” alisema na kuongeza;

“Mbali na hayo wanafamilia mjue kwamba Serikali ipo pamoja na nyinyi, tumeumia pamoja hakuna namna yoyote ya kuweza kuhalalisha utoaji wa haki ya mtu katika mazingira yoyote kwa mtu yoyote kwani nchi inaendeshwa Kwa mujibu wa Katiba na Sheria.”

Aidha Waziri Masauni alisisitiza kwamba; “Sisi zote tumeumbwa na Mwenyezi Mungu na yeye ndiye aliyempangia kila mtu kwamba safari yake iko lini na ataondoka kwa sababu gani, nawaomba sana tuwe na moyo wa subra katika kipindi hiki kigumu, kwani kinachoweza kumsaidia mzazi wetu kwa sasa ni dua na Mwenyezi Mungu amjaalie safari yake iwe nyepesi na sisi Mwenyezi Mungu atujaalie mwisho mwema,”

Wakati huo huo Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limeeleza kupokea kwa kwa mshtuko na kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Kibao.

“TEF tumejiepusha kutoa matamko yanayohusiana na masuala ya kisiasa, tukiamini kwenye siasa vipo vyama vya siasa vyenye jukumu hilo, na jukumu letu la msingi linabaki kuwa la kukusanya, kuchakata na kusambaza taarifa bila kujali mipaka ya nchi.

“Tunawapa pole familia ya ndugu Kibao, Mwenyekiti wa CHADEMA na wana- CHADEMA wote kwa kuondokewa na kiongozi wao katika mazingira ya kusikitisha, na Watanzania wengine waliofikwa na madhila ya namna hiyo,” ilieleza taarifa ya TEF,” alieleza taarifa hiyo.

TEF imesema Wakati unasubiriwa uchunguzi aliouagiza Rais Samia na ombi lao ni kutaka kuunda Tume ya Majaji, ambao wanaamini wamekuwa mstari wa mbele kusimamia haki katika nchi yetu.

Kibao, aliyekuwa Mjumbe wa Sekretarieti ya Chadema alichukuliwa jioni ya Septemba 6, 2024 eneo ya Kibo Complex Tegeta jijini Dar es Salaam na watu wasiojulikana, akiwa safarini kutoka Dar es Salaam kuelekea Tanga na basi la Tashriff na mwili wake kupatikana jana Jumapili Septemba 8, 2024 eneo la Ununio, Dar es Salaam.