July 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei. Picha na IRNA

Khamenei: Iran tupo imara, hatuogopi adui

TEHRAN, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu,Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema kutomuogopa adui na kusimama kidete dhidi yake ni katika maamrisho na maelekezo muhimu ya Qurani Tukufu.

Ali Khamenei aliyasema hayo mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa Musalla wa Imam Khomeni mjini Tehran ikiwa ni siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.

“Leo hii, hali ya kudhalilishwa baadhi ya mataifa ya Kiislamu na madola ya kidhalimu duniani imetokana na kuogopwa maadui wa Uislamu.

“Kuigopa Marekani kuna matokeo machungu na haya tumeyashuhudia katika miaka ya nyuma, ambapo mwenendo wa baadhi ya viongozi wetu kuiogopa Marekani kuliwasababishia matatizo.

“Njia pekee ya kuinusuru jamii ya wanadamu kuondokana na dhuluma, ubaguzi, uonevu, vita, ukosefu wa usalama na kutoheshimiwa thamani za kiutu ambako kumeshuhudiwa katika kipindi chote cha historia ni kufuata kivitendo mafundisho ya Qurani Tukufu,”alifafanua.

Ali Khamenei alisisitiza kuwa, Qurani ni kitabu cha maisha na iwapo wanadamu watashikamana na sheria zake, bila shaka watapata baraka na ufanisi hapa duniani na kesho Akhera.

Pia alieleza wazi kuwa, iwapo sheria za maisha ya dunia zitajengeka katika misingi ya uchu wa kusaka nguvu, fedha na matamanio, basi mwanadamu hatapata furaha katika maisha ya dunia na ya kesho Akhera.

Alibainisha kuwa, Qurani Tukufu imemfudisha mwanadamu kutumia utajiri na uwezo wake wote kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wanadamu wenzake na kuwasaidia watu wenye mahitaji katika jamii.

Hata hivyo,mbali na kiongozi huyo kutoa mkono wa heri na fanaka kwa Waislamu wote kote duniani kwa kuanza mwezi mtukufu wa Ramadhani, aliuasa umma wa Kiislamu kujinyenyekesha kwa Mola na kuendelea kutenda mema.