January 1, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kesi ya mchungaji aliyebaka binti darasa la sita kuendelea Desemba 7

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

KESI ya ubakaji inayomkabili Mchungaji wa kanisa la kilokole la PGM Wilayani
Mbinga Mkoa wa Ruvuma Boston Chimalilo aliyefikishwa katika Mahakama ya Wilaya hiyo kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi wa darasa la sita mwenye umri wa miaka 13 imeahirishwa hadi Desemba 7.

Mwendesha mashtaka wa Polisi, Hamad Mwalimu amedai mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya Wilaya ya Mbinga, Christina Haule kuwa, mshtakiwa huyo Boston Chimalilo ambaye ni mchungaji wa kanisa la kilokole la PGM mwenye umri wa miaka 72, alitenda kosa hilo Desemba Mosi mwaka huu katika maeneo ya makaburi ya Misheni, Mbinga mjini.

Inadaiwa kuwa, mshtakiwa Chimalilo alimchukua mtoto huyo wakati akiwa katika mazingira ya shule huku akiwa amevalia sare zake na kwenda naye katika Makaburi hayo na kisha kumvua nguo na kumbaka.

Wakati akieendelea kutekeleza unyama huo, mwanafunzi huyo alipiga mayowe kuomba msaada na wajitokeza wasamaria wema waliokuwa wakichimba kaburi kwa ajili ya mazishi.

Baada ya kuwaona watu hao wakija eneo alilopo alikimbia na bahati nzuri vijana hao walimkimbiza na kumkamata lakini kwa bahati mbaya alikuwa ameshatekeleza kitendo hicho cha ukatili.

Hata hivyo mshtakiwa huyo amekana mashtaka na amerudish wa mahabusu baada ya kunyimwa dhamana hadi Desemba 7 mwaka huu ambapo kesi hiyo itakapofika mahakamani kwa ajili ya kutajwa.