November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kesi ya mauaji ya Asimwe,kuhamishiwa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba

Na Ashura Jumapili Majira online Kagera,

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera, imefunga rasmi mwenendo kabidhi kuhusu shauri namba 17740 la mwaka 2024,kesi ya mauaji ya mtoto Noela Asimwe Novart mwenye umri wa miaka (2.5).

Shauri hiyo linalowakabiri washitakiwa tisa akiwemo aliyekuwa Padri wa kanisa Katoliki Jimbo la Bukoba pamoja na baba mzazi wa mtoto Noela Asimwe Novart,ambaye aliuawa na kukatwa mikono kisha mwili wake kutelekezwa katika karavati lililoko barabara ya Ruhanga.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Bukoba Elipokea Yona, amesema,mahakama hiyo imefunga kabidhi mwenendo wa shauri hilo la kosa la mauaji linalowakabiri washitakiwa tisa.Hivyo inapelekwa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba.

Ambapo Hakimu Yona, hakutaja tarehe nyingine ya kusikilizwa kesi hiyo,kwa madai kuwa wanasubiri maelekezo ya Mahakama Kuu, hivyo washitakiwa watajulishwa.

Mwendesha Mashitaka wa Mkoa wa Kagera,Waziri Magumbo,kwa kushirikiana wa mawakili wenzake wanne wa serikali akiwemo Erick Mabagala,walisoma maelezo yaliyotolewa na mashaidi 52.Kisha kutoa vielelezo 37,kati ya hivyo 27 ni nyaraka na kumi ni vielelezo vya kushikika ikiwemo mifupa miwili ya marehemu Noela mbele ya Mahakama hiyo.

Magumbo amesema,kilichokuwa kinafanyika tangu shauri hilo kufikishwa mahakamani hapo ni kujilidhisha chini ya kifungu cha sheria 246 ya mwenendo wa makosa ya jinai.Ambapo upelelezi ukikamilika ,washtakiwa wanatakiwa kusomewa ushahidi na mashahidi watakaowasilishwa wakati wa kesi baada ya kupelekwa Mahakama Kuu yenye mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.

Hata hivyo aliwataja washtakiwa wanaokabiliwa na shitaka hilo,kuwa ni Elpidius Rwegoshora,aliyekuwa Padri wa Jimbo Katoliki la Bukoba ambaye ni mshtakiwa namba moja na Novath Venant baba mzazi wa mtoto Noela.

Huku washtakiwa wengine ni Nurdin Masoud, Ramadhan Selestine, Rwenyagila Alphonce, Dastan Burchard, Faswiu Athuman, Gozibath Archard na Dezdery Everigist.

Magumbo amesema, kesi hiyo ilifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Bukoba Elipokea Yona kwa mara ya kwanza Juni 28,2024.

Amesema, Mei 30,mwaka huu, mtoto Noela aliibwa na watu wasiojulikana, ambao walifika nyumbani kwao marehemu huyo na kumpora mikononi mwa mama yake kisha kutokomea kusikojulikana.Juni 17,mwaka huu mwili wa Noela ulipatikana ukiwa umetelekezwa katika karavati lililoko barabara ya Ruhanga ukiwa umekatwa mikono.

Washtakiwa wote tisa, jana walisimama pekee yao baada ya Hakimu kuwauliza kama wanajambo la kueleza.Ambapo mshitakiwa namba moja Elpidius Rwegoshora ,namba mbili Novath Venant,tatu Nurdin Masud,tano Rwenyagira Alfonce,saba Dunstan Burchard ,nane Gozbart Arikad na namba tisa Dezideri Everigist , walisema wataleta mashahidi wakati kesi yao itakapoanza kusikilizwa.

Huku mshtakiwa namba nne na sita hawana mashahidi ingawa mshtakiwa namba moja anatetewa na Mawakili wawili ambao Mathias Rweyemamu na Pontian Mujuni.