Na Magreth Kinabo–Mahakama
MAHAKAMA ya Tanzania imefanikiwa kuendesha mashauri 4,711 kwa njia ya Mahakama Mtandao maarufu kama ‘Video Conference’ ikiwa ni hatua mojawapo za kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona (COVID-1 9) katika kipindi cha miezi miwili.
Mashauri hayo yamesikilizwa kwa njia hiyo, kufuatia utekelezaji wa agizo la Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Ibrahim Juma alilolitoa Machi 23, mwaka huu la kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuwaepusha watumishi wa Mahakama, Magereza, wafungwa na mahabusu na wateja wengine wa Mahakama dhidi ya maambukizo hayo, wakati shughuli za utoaji haki zikiendelea kufanyika.
Agizo hilo lilitolewa na Prof. Juma kupitia mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika jijini Mwanza, la kuongeza kasi ya matumizi ya TEHAMA kwenye kipindi hiki ambacho taifa na dunia mzima kukumbwa na janga la ugonjwa huo.
Akizungumzia kuhusu usikilizaji wa mashauri kwa kutumia teknolojia hiyo, Mkurugenzi Msaidizi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Machumu Essaba amesema imelipunguzia pia Jeshi la Magereza gharama za usafiri wa kila siku za kuwaleta wafungwa au mahabusu mahakamani na msongamano
‘‘Njia hii imetumika katika kipindi cha ugonjwa huu, kuanzia Machi 23, mwaka huu hadi Mei 26, mwaka huu, ambapo Mahakama ya Rufani Tanzania, imesikiliza mashauri 48 kupitia vikao vitano, kati ya hivyo vitatu vilifanyika katika Jiji la Dar es Salaam, vilivyohusisha mashauri 30 na kimoja Tabora kilichohusisha mashauri tisa na kingine Iringa kilichokuwa na mashauri tisa,’’ amesema Essaba.
Amesema kuwa, Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam imesikiliza mashauri 3,188 kati ya hayo, mashauri 804 yamesikilizwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mahakama za Wilaya, Kinondoni 714, Ilala 992, Temeke 523, na Kigamboni 155.
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya, Mahakama ya Mkoa na Wilaya mashauri yaliyosikilizwa kwa teknolojia hiyo ni 367, kanda zingine ni Tanga 310, Musoma 158, Tabora 130, Dodoma 78, Mtwara 66, Moshi 46, Arusha 41, Kigoma, 37, Sumbawanga 23, Iringa 15, Songea 14, Shinyanga 12, Mwanza 28 na Bukoba 5.
Essaba amefafanua kwamba, Mahakama Kuu Divisheni za Biashara imesikiliza mashauri 55 na Kazi mashauri 90, ambazo zilitumia vifaa vilivyopo kwenye maeneo yao.
Aidha, ameongeza kwamba, zaidi mashauri 300 yamesikilizwa na Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza kwa kutumia simu ya mezani ‘Teleconference’ kwa sababu kuna tatizo la ukosefu wa huduma ya mtandao ‘internet’ kwenye ofisi za Mwanasheria wa Serikali, hali inayosababisha kutumia njia hiyo.
Uongozi wa Mahakama katika kuunga mkono juhudi za Serikali kukabiliana na virusi vya Corona ulikabidhi vifaa vya TEHAMA kwa Maafisa TEHAMA wa kanda 16 za Mahakama Kuu Aprili 21, mwaka huu ili kuziwezesha Mahakama nyingine kuanza kusikiliza mashauri kwa Mahakama Mtandao.
Awali teknolijia hiyo ilikuwa inatumika katika vituo sita, ambavyo ni mfumo huo, umefungwa ambavyo ni Mahakama Kuu ya Tanzania katika Kanda za Dar es salaam, Mbeya, na Bukoba pamoja na Kituo cha Mafunzo cha Kisutu, Gereza la Keko na Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA), Lushoto.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa