April 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

KCBL yatenga Bil 3.5/- za ununuzi wa kahawa

Na Kija Elias, TimesMajira,OnlineMoshi.

BENKI ya Ushirika Mkoani Kilimanjaro (KCBL), imetenga kiasi cha sh. bilioni 3.5 kwa ajili ya maandalizi ya ununuzi wa kahawa kwa msimu wa mwaka 2021/22.

Meneja Mkuu wa KCBL Mkoa wa Kilimanjaro, Godfrey Ng’urah, ameyasema hayo jana katika Mkutano Mkuu maalumu wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa Kilimanjaro KNCU (1984) Ltd, uliofanyika katika hoteli ya chama hicho uliopo mjini Moshi.

Ng’urah amesema Benki ya Ushirika KCBL kwa mwaka huu imetenga sh bilioni 3.5, na kwamba tayari wameshatoa kiasi cha sh. milioni 600 kwa ajili ya manunuzi na makusanyo ya kahawa ili kuwawezesha wakulima kuongeza uzalishaji wa zao la kahawa mkoa Kilimanjaro.

“KCBL kwa mwaka huu pekee imetenga zaidi ya sh. bilioni 3 kwa ajili ya kununua Kahawa na hadi sasa tumeshatoa zaidi ya sh. milioni 600 kwa ajili ya manunuzi na makusanyo ya kahawa kwa msimu huu,”amesema Ng’urah.

Aidha amesema benki hiyo pia imelenga kuongeza uzalishaji wa kahawa katika kipindi cha miaka miwili ijayo kutoka tani 1500-2000 mwaka 2020 hadi kufikia tani 5000-6000 ifikapo mwaka 2024.

“Wenzetu wa mkoa wa Kagera KDCU na KCU nwaka 2020 walizalisha tani 13,000 ukilinganisha na sisi ambao tulizalisha tani 1,500 ambacho ni kiwango cha chini sana,”amesema.

Naye Meneja wa Benki ya Ushirika Tawi la Moshi, Bonaventura Lupindu, amesema katika kukuza uzalishaji wa kahawa kwa kila mkulima atakayefungua akaunti ya KCBL, atapatiwa miche ya kahawa ili aweza kwenda kuipanda.

“KCBL imekuja na bidhaa za ziada kwa wateja wetu, vyama vya Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro, wateja wa KCBL, taasisi na mashirika ya umma wataweza kupatiwa huduma hiyo,”amesema.

Lupindu amesema benki ya ushirika kwa kushirikiana na bodi ya zao la kahawa nchini (TCB) wamesaini mpango mkakati wa kuinua uzalishaji wa zao la kahawa mkoa Kilimanjaro ambapo wakulima watapatiwa miche ya kahawa kadri ya mahitaji yao.

Amesema benki ya ushirika imeandaa bidhaa mahusisi za kuongeza uzalishaji wa kahawa kwa kutoa mikopo ya mbolea,magunia na madawa kwa mwanachama mwenye akaunti KCBL.

Amesema KCBL inatoa mikopo ya uwezeshaji wa ununuzi na uuzaji wa kahawa kwa vyama vya msingi vya ushirika vya mazao Amcos kwa riba rafiki na masharti nafuu kwa msimu 2021/2022