November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kazikazi Family yazidua filamu mpya

Na Bakari Lulela,TimesMajira Online

KIKUNDI cha Sanaa za maigizo Kazikazi Family, kilichopo kata ya Sandari Temeke jijini Dar es Salaam, kimezindua Filamu inayoitwa ‘Serikali Mpya’ inayosapoti juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli katika kudumisha sekta ya Sanaa na michezo nchini.

Uzinduzi huo umefanyika chini ya mgeni rasmi mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo Suleiman Zuberi ambaye amemuakilisha diwani wake, amewapongeza wasanii kwa kufikia hatua hiyo na kuwataka kujituma zaidi kupiga hatua katika sekta ya sanaa.

Zuberi amesema, Serikali ya kata imeandaa program mahususi kwa ajili ya kuwasaidia na kuwashika mkono vijana wenye vipaji vya aina mbalimbali ili kutimiza malengo ya fani zao ikiwemo waigizaji, waimbaji, wachoraji, wachezaji wa mpira wa miguu na mikono ili waweze kujiajiri kupitia vipaji vyao.

Akizungumza katika uzinduzi huo, kiongozi huyo wa mtaa amesema kufuatia hatua waliofikia kama kikundi cha Kazikazi Family kucheza picha yenye maudhui makubwa ya kuipongeza serikali umoja wao uendelee hivyohivyo ili kuiletea heshima kata hiyo kupitia fani ya uigizaji.

“Serikali kuu inatambua mchango wenu kama wasanii, juhudi mbalimbali zinafanyika dhidi yenu kuhakikisha kuwa fani ya sanaa inakuwa yenye manufaa kwa kujiajiri na kuwafanya wasanii kuwa na maisha bora kupitia tasnia hii,” amesema Zuberi.

Mkuu huyo amewataka wasanii kujipanga na fursa mbalimbali za maka 2021 ambayo itakuwa na neema kwa makundi ya sanaa na wasanii ikiwa pamoja na kuwekewa mikakati ya kuwafanya vijana kuondokana na makundi ya uhalifu, utumiaji wa madawa za kulevya, uporaji na matendo ya anasa.

Kwa upande wake meneja wa Kazikazi Family Rashidi Hamza Gila maarufu kama ‘Gilaboy’ amewaambia wapenzi na mashabiki wa filamu kuipokea kwa mikono miwili filamu hiyo bora yenye kuielimisha jamii mwenendo bora wa maisha.

Amesema, Serikali mpya imekuja kuwapa matumaini mapya na kuwataka vijana kuwa makini katika masuala ya maisha kuondokana na utegemezi ambayo ni adui wa maendeleo kwa jamii za watanzania hususani vijana.

Gila boy amesema, Filamu ya ‘Serikali Mpya’ imeandaliwa kwa kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya tano ya kuwataka vijana kujiajiri sio kutegemea ajira kutoka Serikali na sekta binafsi, katika filamu hiyo wameshirikishwa wasanii maarufu kama Bambo na Full tank.

Naye msanii Anifa Daudi Biswaga ambaye ni mtu mwenye ulemavu wa miguu katika filamu hiyo amecheza kama ombaomba ambapo ameeleza, kundi hilo la wenye ulemavu wanafursa sawa kama walivyo watu wengine hivyo wanatakiwa kujiamini na kuacha tabia za kuomba pia jamii iwaheshimu.