January 17, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kaze: Hatutakurupuka kusajili

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

USHINDI wa mabao 5-0 walioupata Yanga katika mchezo wao wa juzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Mwandui FC uliochezwa katika Uwanja wa CCM Kambarage uliopo Shinyanga, umebadili mawazo ya kocha mkuu wa timu hiyo, Cedric Kaze ambaye sasa atalazimika kurudi tena na kukaa meza moja na viongozi ili kuangalia upya majina ya nyota wake aliopanga kuwaacha.

Toka kocha alipochukua mikoba ya Zlatko Krmpotic, timu yake ilikuwa haijawahi kupata ushindi mnono wa goli nyingi jambo ambalo lilikuwa likimuuza kichwa ni namna gani ataweza kuondokana na tatizo hilo na kuipatia makali safu yake ya ushambuliaji ambayo ilikuwa ikipoteza nafasi nyingi za kufunga.

Jambo hilo lilimfanya kocha huyo ambaye alikuwa hataki kugusia jambo lolote la usajili kuweka wazi kuwa anahitaji kufanya usajili ili kuboresha eneo hilo kwa kuwaongezea mtu ambaye ataziba pengo hilo na atafanya wawe na ushindani.

Sababu hizo zilimfanya Kaze kumuagiza haraka mshambuliaji wao Said Ntibazonkiza ili kumuangalia kama atakuw ana muunganiko mzuri na wenzake ambao aliamua kuwapa nafasi ya mwisho ya kuonesha uwezo wao kabla ya dirisha kufunguliwa na ikiwa watashindwa kubadilika basi atalazimika kutafuta wazu watakaoziba nafasi zao.

Lakini baada ya mchezo dhidi ya Mwadui ambao magoli ya Yanga yalifungwa na Deus Kaseke dakika ya sita na Yacouba Sogne dakika ya 14 na 49 jambo ambalo linaelezwa ni moja na sababu mchezaji huyo akasalia ndani ya kikosi hicho baada ya awali kukalia kuti kavu na kuwa miongozi mwa wachezaji ambao wangekatwa kutokana na kushindwa kutumia ipasavyo pasi za mwisho za magoli.

Goli hizo mbili alizofunga dhidi ya Mwadui zinamfanya Yacouba kufikisha goli tatu huku akifanikiwa kutengeneza pasi za mwisho za magoli nne.

Magoli mengine katika mchezo huo yalifungwa na Tuisila Kisinda dakika ya 57 na Lamine Moro Dakika ya 70 yaliyowaimarisha Yanga kileleni mwa msimamo wa Ligi baada ya kufikisha pointi 37, kocha huyo amekuja na mpango tofauti.

Amesema, kilichomfurahisha ni wachezaji wake kufanikiwa kuchukua alama tatu muhimu katika mchezo huo pamoja na kiwango bora kilichooneshwa na wachezaji wake a mbao sasa anaamini watafanya vizuri zaidi katika mechi zao zijazo kwani magoli matano ambayo wameyafunga yatawaongezea kujiamini zaidi.

Kutokana na kuridhishwa na muunganiko walionao wachezaji wake, sasa atalazimika kukutana na viongozi ili kuangalia kama wana haja ya kuongeza mchezaji au kuendelea na hawa alionao sasa.

Amesema, ikiwa wataongeza mchezaji basi ni lazima awe na manufaa makubwa ikiwemo kuongeza kitu ndani ya kikosi chake na kufanya usajili kwa wasiwasi kutokana na kile kinachozungumzwa na watu.

“Hatutafanya usajili kwa kukurupuka au kwa kile watu wanachosema bali tutakaa chini na viongozi na kuangalia ni nafasi gani tuna shida ya kuongeza mchezaji na ikiwa tutaona hawa tulionao wanatosheleza kile tunachokihitaji basi huenda tusifanye usajili, ” amesema Kaze.