January 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kaya 19,530,Arusha kufikiwa na nishati safi ya kupikia

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online,Arusha

WAKALA wa Nishati Vijijini (REA),imeingia mkataba na mtoa huduma kampuni ya Lake Gas Limited kwa ajili ya kutekeleza mradi wa sh. milioni 406.7,wa kusambaza majiko ya gesi ya kupikia(LPG), 19,530 ya kilo sita kwa bei ya ruzuku ya asilimia 50.

Ambapo majiko hayo yatauzwa katika maeneo ya vijijini ndani ya Wilaya ya Arusha, Karatu, Longido, Meru, Monduli na Ngorongoro mkoani Arusha.

Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji Miradi REA, Mhandisi Emmanuel Yesaya,amebainisha hayo mwishoni mwa wiki mkoani Arusha wakati akimtambulisha mtoa huduma katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

“Tumeanza utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034,ambao unasisitiza miaka 10 kutoka sasa asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia, na hili linaweza kufikiwa kupitia mbinu na mikakati mbalimbali ikiwemo hii ya usambazaji wa majiko ya gesi kwa bei ya ruzuku,”amesema Mhandisi Yesaya.

Amefafanua kuwa, REA imeandaa programu mbalimbali ili kufanikisha adhma hiyo ya Serikali ambayo imeasisiwa na Rais  Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kulinda afya za wananchi wake sambamba na kuhifadhi mazingira kwa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Amesema, lengo la mradi huo ni kukuza, kuchochea, kuwezesha na kuboresha upatikanaji wa huduma za nishati safi ya kupikia ili kupunguza ukataji miti ambapo alibainisha kuwa takribani hekta 400,000 hukatwa kila mwaka.

“Mradi huu unakwenda kusaidia kuondokana na athari za kiafya, pia utasaidia kuepuka vitendo vya kikatili, kulinda vyanzo vya maji na kutunza mazingira,pia kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa inayosababisha mabadiliko ya tabianchi,”amefafanua Mhandisi Yesaya.

Vilevile amesema,mradi huo ni nyenzo muhimu ya kupunguza umaskini miongoni mwa jamii za maeneo ya vijijini, kwani utatoa fursa kwa wanawake kujikita katika shughuli za uzalishaji mali pindi wanapotumia mitungi ya gesi kama njia mbadala ya kupikia sababu inaokoa muda ikilinganishwa na matumizi ya kuni na mkaa.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Missaile Musa,amesema mpango huo,utawasaidia wananchi ambao hawana uwezo wa kumudu gharama ya manunuzi ya majiko hayo ya gesi.

“Ninaamini kwa ruzuku hii iliyowekwa na Serikali,wananchi wengi watamudu gharama na itafanikisha lengo la asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034,”amesema.

Naye Meneja Masoko wa Kampuni ya Lake Gas, Kanda ya Kaskazini, Ismail Juma amethibitisha kuwa wamejipanga vyema kuhakikisha wanufaika wa majiko hayo wanafikiwa.Huku akitoa wito kwa wananchi mkoani humo kuchangamkia fursa hiyo iliyotolewa na Serikali kupitia REA.

Ametoa rai kwa wananchi kutimiza masharti ya kupata majiko hayo ya ruzuku ikiwa ni pamoja na kuwa na kitambulisho cha Taifa (NIDA) ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa kila mwananchi.

Wakala wa Nishati Vijijini unatekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034 ambao ulizinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan Mei mwaka huu.