Na Isaack Zenda, Timesmajira
MWENYEKITI wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Mohammed Kawaida ameongoza hafla ya uzinduzi wa Kijani Ilani Chat Bot, programu mpya ya kidijitali inayolenga kuongeza hamasa za kisiasa miongoni mwa vijana kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Kawaida amesema kuimarishwa kwa kampeni za kidijitali ni hatua muhimu katika kuhakikisha vijana wanajitokeza kwa wingi kushiriki zoezi la upigaji kura.
“Teknolojia hii mpya itakuwa nyenzo muhimu kwa vijana kupata taarifa sahihi za Ilani ya Chama, kujua vipaumbele na sera zetu, na hatimaye kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi,”amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti Mwenza wa UVCCM Taifa, Khalid Mwinyi, amesisitiza umuhimu wa chat bot hiyo katika kuimarisha uelewa wa vijana.

“Tunatambua kuwa tunakaribia uchaguzi mkuu, hivyo kampeni za kidijitali ni nyenzo isiyoepukika. Kupitia Kijani Ilani Chat Bot, vijana watapata fursa ya kujifunza na kuelewa zaidi dira ya chama chetu kuelekea uchaguzi,” amesema.
Aidha, Kawaida amewataka vijana kuendelea kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mgombea Urais kupitia CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na mgombea mwenza wake, Emmanuel Nchimbi, akiwapongeza kwa hatua ya kuchukua fomu za kugombea nafasi hizo.

Katika hotuba yake, pia alimpongeza Katibu Mkuu mpya wa UVCCM Taifa kwa kuaminiwa na chama na kuweka historia ya kuwa kiongozi mdogo zaidi kushika wadhifa huo.
“Katibu wetu mpya, umeandika historia na umetupa matumaini makubwa kwamba lolote linawezekana. Ni wajibu wako sasa kuhakikisha unawaunganisha vijana na kuwaongoza kutumia ipasavyo programu hii mpya ya Ilani ya Chama,” amesema.

Akihitimisha hotuba yake,Kawaida amewataka vijana kupuuza upotoshaji wa kimtandao unaohusishwa na maandamano, na badala yake wajikite katika maandalizi ya kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba.

“Ni wajibu wa kila kijana kuhakikisha anajitokeza kupiga kura. Tuwape mkono Rais wetu na chama chetu kwa vitendo,”amesisitiza.
Mwisho, amewashukuru vijana wote waliohudhuria hafla hiyo kwa mshikamano na mwamko wao katika kuunga mkono jitihada za chama kupitia nyanja za kidijitali.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi