January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Katibu Mkuu Wizara ya Nishati apongeza Watumishi Wizara na Taasisi kwa utekelezaji wa miradi

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amepongeza Watumishi wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake kwa kuendelea kufanya kazi kwa weledi na bidii ili kuhakikisha kuwa miradi mbalimbali ya Nishati inaendelea kutekelezwa licha ya changamoto zinazoikumba Dunia ikiwemo Uviko-19 na Vita ya Urusi na Ukraine.

Katibu Mkuu ametoa pongezi hizo tarehe 24 Mei, 2022 wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati unaofanyika jijini Dodoma ambao unajadili na kuidhinisha Bajeti ya Wizara ya Nishati kwa mwaka 2022/2023. Mkutano huo umehudhuriwa viongozi mbalimbali wakiwemo Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Wizara ya Nishati, Ziana Mlawa, Mwakilishi wa Katibu Mkuu TUGHE Taifa, Meshack Lugeiyamu na Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Wizara ya Nishati, Zghambo Chinula.

“Nawashukuru na kuwapongeza kwa jitihada ambazo mnaendelea kuziweka katika kazi, nafahamu Wizara hii inashughulika na masuala mengi makubwa pamoja na maisha ya watanzania, tukiwa na udhaifu wowote utaonekana mapema, lakini mnajitahidi kufanya kazi kwa weledi na bidii na kuna miradi mingi ambayo tunaendelea kufanikisha vizuri.” Amesema Katibu Mkuu

Alitaja miradi inayoendelea kutekelezwa na Wizara ya Nishati ni pamoja na mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) ambao umefikia asilimia 60, utekelezaji wa mradi wa Bomba la Mafuta kutoka Uganda ambao unaendelea vizuri  kwa pande zote za Uganda na Tanzania, ambapo kwa Tanzania wananchi wameshalipwa fidia, kazi za kuandaa maeneo ya kupitisha mabomba zinaendelea na muda si mrefu mabomba yatakayopitisha mafuta hayo yataanza kuchomelewa.

Kuhusu mradi wa kusindika Gesi Asilia kuwa kimiminika (LNG) ameeleza kuwa, timu kutoka Wizara ya  Nishati na Taasisi nyingine za Serikali pamoja na wawekezaji wanaendelea na majadiliano ambapo makubaliano ya mwanzo ya mradi huo yanatarajiwa kufikiwa kati ya Mwezi Mei na Juni mwaka huu.

Ameongeza kuwa, Wizara imeongeza nguvu na usimamizi katika kuhakikisha kuwa gesi inayopatikana nchini inaendelea kutumika kwa matumizi mbalimbali ikiwemo majumbani na kwenye magari ambapo Serikali imeshakaa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA)  ili kuweza kuwa na vituo zaidi vya kujazia Gesi ambapo Taasisi  binafsi pia zinapewa kipaumbele.

Ameeleza kuwa, kwa sasa TPDC wanajenga kituo kikubwa cha kujazia Gesi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo malori makubwa yatakuwa yanachukua gesi na kusambaza kwenye vituo nvingine.

Pia amesema TPDC wanajenga vituo katika maeneo  mbalimbali ikiwemo eneo la Feri, Muhimbili, Kibaha na Ubungo yote hiyo ikiwa ni jitihada za kuhakikisha kuwa wananchi wanakuwa na wigo mkubwa wa  kutumia Gesi hiyo, ameongeza kuwa, Wizara ya Nishati itaonesha mfano kwani inatarajia kuwa magari yote ya Wizara yatabadili mfumo ili yaweze kutumia Gesi.

Kuhusu suala la mafuta, amesema kuwa Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA) na EWURA wanafanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha kuwa nchi inakuwa na mafuta ya kutosha na  amezitaka Taasisi hizo kuendelea kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na uaminifu.

Kuhusu usambazaji wa umeme vijijini amesema kuwa, Serikali inaendelea kuweka jitihada ili wananchi waendelee kusambaziwa umeme licha ya kupanda kwa bei ya alminium na shaba kutokana na Vita ya Ukraine na Urusi  kwani nchi hizo ndio wasambazaji wakubwa wa bidhaa hizo zinazotumika kwenye miundombinu ya umeme. Amesema kuwa lengo la Serikali ni vijiji vyote kusambaziwa umeme ifikapo Desemba mwaka huu.

Katika Mkutano huo, Katibu Mkuu amewataka watumishi wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kuweza kuacha alama chanya katika maeneo yao ya kazi na pia ametaka kila mtumishi ahakiksihe kuwa eneo la kazi linakuwa ni eneo lenye furaha ili kuweza kutumikia nchi vizuri na pia kujisomea ili kuendana na mabadiliko ya Teknolojia.

Kwa upande wake, Mwakilishi kwa Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa, Meshack Lugeiyamu amempongeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati kwa kuwa na ushurikiano mzuri na Watumishi wa Wizara na pia kwa usimamizi wa karibu wa miradi mbalimbali Nishati.

Lugeiyamu pia amewaasa Watumishi wa Wizara ya Nishati na Taasisi kutouangusha uongozi wa Wizara ya Nishati katika jitihada zake za kutekeleza miradi mbalimbali ya Nishati.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TUGHE, Tawi la Wizara ya Nishati, Zghambo Chinula amepongeza Serikali kwa kupandisha  mishahara ya wafanyakazi kwa asilimia 23 pia ameupongeza uongozi wa Wizara ya Nishati kwa kujali maslahi ya Wafanyakazi ambayo ni chachu ya Wafanyakazi kuendelea kufanya kazi kwa ari na tija.

Chinula pia ametoa wito kwa uongozi wa Wizara kuendelea kusimamia suala la matumizi ya gesi  ikiwemo kwenye magari kwani suala hilo litaleta unafuu kwa wananchi watakaotumia mfumo huo kwani gharama za uendeshaji wake ni ndogo kulinganisha na mafuta.

 Aliahidi kuwa watumishi wa Wizara ya Nishati wataendelea kutoa ushirikiano kwa Uongozi wa Wizara na kuendelea kutekeleza kwa vitengo dhana ya “Kazi Iendelee” ikizingatiwa kuwa nishati ni injini maendeleo ya nchini.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba akiwa katika Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati unaofanyika jijini Dodoma. Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Wizara ya Nishati, Ziana Mlawa na Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Wizara ya Nishati, Zghambo Chinula. Kulia kwake ni Katibu wa Baraza la Wafanyakazi Wizara ya Nishati, Fortunata Getele na   Mwakilishi wa Katibu Mkuu TUGHE Taifa, Meshack Lugeiyamu.
Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Wizara ya Nishati, Zghambo Chinula akizungumza katika Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati unaofanyika jijini Dodoma. Wa Tatu kutoka kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Wa Pili kulia ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Wizara ya Nishati, Ziana Mlawa.  Wa Kwanza kushoto ni Katibu wa Baraza la Wafanyakazi Wizara ya Nishati, Fortunata Getele.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati. Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Wizara ya Nishati, Ziana Mlawa na Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Wizara ya Nishati, Zghambo Chinula. Kulia kwake ni Katibu wa Baraza la Wafanyakazi Wizara ya Nishati, Fortunata Getele na   Mwakilishi wa Katibu Mkuu TUGHE Taifa, Meshack Lugeiyamu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Sekretarieti ya Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati unaofanyika jijini Dodoma. Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Wizara ya Nishati, Ziana Mlawa na Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Wizara ya Nishati, Zghambo Chinula. Kulia kwake ni Katibu wa Baraza la Wafanyakazi Wizara ya Nishati, Fortunata Getele na   Mwakilishi wa Katibu Mkuu TUGHE Taifa, Meshack Lugeiyamu.
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati wakiimba wimbo wa mshikamano katika Mkutano Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati unaofanyika jijini Dodoma.
Wajumbe mbalimbali wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati wakiwa katika Mkutano wa Baraza hilo unaofanyika jijini Dodoma.