Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga amehaidi kufanya mabadiliko makubwa ya mfumo wa ukusanyaji mapato yatokanayo na pango la ardhi kama ilivyo mifumo ya kisasa inayotumiwa na mamlaka za maji safi na mazingira hapa Nchini.
‘’Ili kuwa na mafanikio makubwa ni lazima tujue idadi ya wamiliki wa ardhi nchini kwa kuwaingiza kwenye mifumo ili tuweze kujua kiwango cha mapato yatokanayo na kodi ya ardhi hapa Nchini.’’Alisisitiza Katibu Mkuu mteule Wizara ya Ardhi Mhandisi Anthony Sanga.
Mhandisi Sanga amesema hayo leo tarehe 28 Februari wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya ofisi kati yake na Katibu Mkuu anayemaliza muda wake Dkt. Alla Kijazi kufuatia kuteuliwa kwake kuongoza Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi uteuzi uliofanywa hivyi karibuni na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akitoa uzoefu wake katika mifumo ya ukusanyaji mapato kupitia Wizara ya maji na mamlaka zake Mhandisi Sanga amesema walifanikiwa kuwa na mifumo imara baada ya kuachana na mifumo kutoka nje ya nchi na kuwaamini wataalam wa ndani ambao wamefanikiwa kutengeneza mifumo imara ya ukusanyaji miamala ya maji.
Ni kwa muktadha huo Katibu Mkuu Sanga akaimiza kutumia wataalam wa mifumo wandani na kuamini watendaji wengine wa sekta ya ardhi kwa kuwapa nafasi ili waweze kuonesha uwezo wao akichagiza kuwa yeye anatabia ya kuamini watu anaofanya nao kazi.
Naye Katibu Mkuu anayemaliza muda wake Dkt. Allan Kijazi amewataka watendaji wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuendelea kufanya kazi kwa karibu na kiongozi huyo mpya ili kuendeleza kazi kubwa ambayo yeye na wenzake wamekuwa wakiendelea nayo hadi sasa wakati anamaliza muda wake.
Dkt. Allan Kijazi aliawataka wajumbe wa Manejimenti ya Wizara kusaidia viongozi wapya Wizarani hapo ili waweze kukabiliana na changamoto zilizopo hususani migogoro ya ardhi kwa kuwapitisha katika yale ambayo washayafanyia kazi na yale ambayo wataendelea kuyafanyia kazi na hatimaye kuja na suluhisho la kudumu katika juhudi za kutokomeza migogoro hiyo.
Dkt. Kijazi aliongeza kuwa tayari Wizara ishaanza kufanyia kazi Migogoro hiyo na kwa kuanzia ilianzia katika Mikoa yenye migogoro sugu ya ardhi na tayari zoezi hilo limekamilika katika mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma na litaendelea kwa Mikoa ya Mwanza na Arusha ikiwa ni hatua muhimu katika kukabiliana na changamoto hiyo.
Akiangazia suala la makusanyo ya kodi ya pango la ardhi Dkt. Kijazi alisema mpaka sasa wastani wa ukusanyaji mapato ya ardhi ni kwa asilimia sitini tu hivyo kumtaka Mhandisi huyo kuboresha namna ya kuingiza wamiliki wa ardhi katika mifumo ili waweze kulipa kodi ya serikali kama inavyotakiwa.
Katibu Mkuu Mhandisi Anthony Sanga pamoja na Naibu Katibu Mkuu wake Lucy Kabyemela mapema leo hasubuhi wamewasili makao Makuu ya Wizara ya Ardhi Mtumba na kupokelewa kwa shangwa na watumishi wa Wizara hiyo tayari kwa kuanza kazi yao leo kufuatia uteuzi wao na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani hivi karibuni.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi