January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Katibu Mkuu Maji aagiza uvunaji wa maji ya mvua

Na Joyce Kasiki ,Timesmajira online,Dodoma

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri  amezindua taarifa ya utendaji wa Mamlaka za Majisafi  na Usafi wa Mazingira kwa kipindi cha mwaka 2022/23 .

Akizungumza jijini Dodoma wakati wa uzinduzi huo kwa niaba ya Waziri wa Maji Jumaa Aweso, ,Mhandisi Waziri ameziagiza Mamlaka za Maji kushirikiana na halmashauri zote nchini katika kuhasisha uvunaji wa maji ya mvua hasa katika kipindi hiki cha mvua zinazoendelea kunyesha.

Amesema katika kipindi hiki cha masika zimenyesha mvua nyingi ambazokatika baadi ya maeneo zimesababisha madhara huku aisema kama maji hayo yatavunwa itapunguza athari  lakini itawezesha wananchikuwa na akiba ya maji.

Amezitaka Mamlaka hizo kusimamia malengo ya Maendeleo Endelevu hasa lengo namba sita linaloeezea umuhimu wa wa maji safi na usafi wa mazingira.

“Lengo namba sita katika malengo ya Maendeleo  Endelevu  linasisitiza kuhakikisha uwepo na usimamizi endelevu wa maji na usafi wa mazingira kwa wote ikiwa ni pamoja na watu wote kuwa na uhakika wa upatikanaji wa majisafi na salama ya kunywa kwa bei nafuu ifikapo mwaka 2030,”amesema Mhandisi Waziri 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Dkt.James Andilile amemuhakikishia Katibu Mkuu huyo kuwa EWURA  itaendelea kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha kuwa katika nchi kunakuwa na huduma  za maji zinazokidhi mahitaji lakini pia ni huduma zenye uhakika na  katika hali endelevu kwa kuhamasisha na kusimamia ufanisi.

Aidha ameelezea mafanikio katika Mamlaka za Maji ambapo amesema , utendaji  umeendelea kuimarika ambapo kwa kipindi cha  2022/23, Mamlaka za Maji 78 kati ya 85 zilipata alama kuanzia wastani hadi vizuri sana katika utendaji wa ujumla ikilinganishwa na mamlaka 77 kati ya 90 kwa mwaka 2021/22. 

Aidha ameshauri  kuwa kasi ya uwekezaji kwenye miundombinu ya majisafi na usafi wa mazingira ziwiane na kasi ya ongezeko la watu katika miji  hapa nchini kwa lengo la kuwa na huduma stahiki kwa wananchi.

Hata hivyo Dkt.Andilile amesema pamoja na kuimarika kwa utendaji kazi wa mamlaka za maji katika kutoa huduma, uchambuzi umebainisha changamoto zinazozikabili mamlaka za maji  ni pamoja na kutokidhi kiwango cha dawa  katika maji yanayosambazwa.

Pia ametaja changamoto nyingine kuwa ni   Majitaka yaliyotibiwa kutokidhi viwango vya ubora kwenye viashiria vya  mahitaji ya oksijeni kibiolojia na kikemikali , Uwiano mdogo wa idadi ya watu wanaopata huduma ya majisafi na usafi wa mazingira,upotevu mkubwa wa maji wa zaidi ya asilimia 20 inayokubalika na uchache wa miundombinu ya miundombinu ya kutibu majitaka na topetaka kinyesi.

Vile vile amesema uwiano mdogo wa uzalishaji wa maji ikilinganishwa na mahitaji,bei za maji za muda mrefu ambazo haziendani na gharama halisi za uendeshaji  na upatikani wa huduma isiyotesheleza ya usafi wa mazingira.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar  (ZURA) Omar Ali Yussuf, , amesema kuwa EWURA imekuwa ikifanya kazi kubwa ambayo inaleta heshima kwa Taifa la Tanzania.